Singida yapokea bilioni 17.85/- kumpa mtoto elimu bora

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Peter Serkamba katika Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) akiwaonesha Wadau Kitabu chenye maelezo ya kina kuhusu Programu hiyo baada ya kukata utepe wa kitabu hicho kuashiria Uzinduzi rami kimkoa.  


Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe (aliye karibu na kamera) akiwa na wadau wengine waliohudhuria uzinduzi wa PJT- MMMAM akisikiliza kwa makini kinachoendelea kwenye hafla hiyo
Bruno Ghumpi, mwezeshaji  kutoka Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Nchini (TECDEN) akitoa mada kwa Wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) uliofanyika kimkoa mjini Singida

Mmoja wa Watoa mada, Isack Idama kutoka Shirika la Watoto walio kwenye Mapambano yaani "Children in Cross fire" (CiC) akitoa mada wakati wa hafla ya Uzinduzi wa PJT- MMMAM kimkoa mjini Singida


 

 

Na Abby Nkungu, Singida

 

SERIKALI imeupatia mkoa wa Singida zaidi ya shilingi bilioni 17.85 kwa ajili ya kuboresha elimu ya awali na msingi  katika kipindi cha mwaka wa  fedha 2021/2022  na 2022/2023.

 

Hayo yalielezwa mjini hapa na Mkuu wa mkoa huo, Peter Serukamba wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT - MMMAM) kimkoa.

 

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, mkuu huyo alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kilitumika kuwezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ya awali na shule za msingi.

 

"Serikali ya awamu ya sita ya Dk Samia Suluhu Hassan imewekeza sana kwenye sekta ya elimu ya awali na shule za msingi katika mkoa wetu. Imewajengea uwezo wa ufundishaji, kutengeneza na kutumia zana, malezi na makuzi kwa walimu 151 wa elimu ya awali, walimu wakuu 21 na maofisa kata 21. Pia utekelezaji wa miradi ya 'BOOST', 'SEQUIP', ujenzi wa shule mpya za msingi na upanuzi wa shule moja" alifafanua.

 

Alisema kuwa lengo la juhudi hizo ni kuhakikisha watoto wanaosoma elimu ya awali na msingi wanakuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia. Pia kuwa na walimu wenye weledi ili kuinua kiwango cha taaluma.

 

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Serikali imewekeza zaidi katika suala la lishe bora, afya na  ulinzi na usalama wa mtoto.

 

“Ili kuhakikisha mtoto wa kitanzania anakua katika utimilifu wake, Serikali imewekeza vya kutosha katika kuboresha uhai wake kupitia utoaji wa huduma bure za afya kwa mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano” alieleza kisha akaongeza;

 

"Lishe ni suala mtambuka; hivyo Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto haina budi kutumika kama fursa ya kutekeleza suala la lishe kwa watoto ili kuondokana na utapiamlo na udumavu usio wa lazima".


Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Yangson Mgogo alisema kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo; hivyo jamii inapaswa kumwandaa mtoto katika misingi na maadili ya Kitanzania kwa kuzingatia matakwa ya  Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.


"Kila umwonaye mwenye tabia na maadili mema, ujue huko chini kazi kubwa imefanyika" alisema kisha akatoa wito kwa jamii yote nchini kuhakikisha inasimamia kikamilifu malezi na makuzi ya mtoto ili hatimaye nchi iwe na Taifa lenye maadili mema.


Sheikh wa Mkoa wa Singida, Sheikh Issa Nassoro alisema mtoto bora ni Taifa  bora; hivyo kila kiongozi wa dini na mzazi ahakikishe analinda na kuwalea watoto katika misingi imara ya Kitanzania.


Naye Katibu Tawala wa Mkoa, Dk Fatma Mganga alisema kuwa malezi bora huleta utii, unyenyekevu na uadilifu; hivyo akawasihi viongozi wa dini kuwalea watoto kiroho kwa kuwa mtoto aliyelelewa kimwili tu hawezi kukua katika utimilifu wake kutokana na kutokuwa na hofu ya Mungu.


Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa wanasema Programu hii ingejielekeza pia kwenye suala la mila na desturi potofu zinazoathiri malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.


Wamezitaja baadhi ya mila hizo kuwa ni pamoja na kurithi wajane, kuzuia baadhi ya vyakula muhimu kwa watoto na  kuwakingia kifua ndugu wanaofanya ukatili dhidi ya watoto; ukiwemo ubakaji, ulawiti na vipigo.


"Kuna baadhi ya makabila ya mkoa wa Singida; hasa maeneo ya vijijini,  wajawazito huzuiwa kula mayai au watoto kukatazwa kula maini kwa madai kuwa. yana athari kiafya" alieleza Kidoho Kidimanda, mkazi wa eneo la Utemini Manispaa ya Singida.


Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT - MMMAM)

ambayo ni ya miaka mitano, ilizinduliwa Kitaifa Desemba 2021 jijini Dodoma ikilenga maeneo matano ya mfumo wa malezi; nayo ni afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama kwa watoto walio na miaka 0 hadi 8. 



This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post