Father on duty: Mkakati mpya wa kutokomeza ukatili wa Kingono kwa Watoto wa kiume Arumeru

Baba wa zamu akiwa kwenye majukumu yake ya kutoa elimu kwa mmoja wa wanafunzi anaowahudumia katika shule ya msingi katika kata ya Kiranyi

 

“Nilipohamishiwa hapa shuleni kama Mwalimu Mkuu miaka sita iliyopita nilikuta baadhi ya Watoto wa kiume wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wengine wakiwa kwenye hali ya hatari sana. Nilijiuliza maswali mengi  ya namna gani nitaweza kuwaokoa watoto hawa  kwenye hili tatizo,”.

 

“Nilijikuta naingia kwenye maombi na sala,  nikiwa namuomba sana Mungu anisaidie niweze kufaniwa kwa kuwa hili tatizo ni hatari sana kwa mustakabali wa maisha yao ya mbeleni hasa ukizingatia vijana hawa ndio tunaowatayarisha kuwa Baba wa familia wa baadae,’’.

 

" Hata hivyo nilifarijika sana siku moja baada ya kupokea ujumbe kutoka Halmashauri yetu ya Arusha ukiongozwa na Afisa maendeleo ya Kata kuwa nimeletewa mradi wa kumsaidia mtoto wa kiume na kumlinda dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti chini ya shirika la Center for Women and Children Development (CWCD). Niliwapokea kwa furaha kubwa nikijua  kabisa sasa tatizo hili litakomeshwa na tutaokoa Watoto wetu,”.

 

Hayo yote si ya mwingine bali ni maneno ya Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kiranyi, Mwalimu Hussein Mamboli ambaye anasema shule yake ni miongoni mwa shule ambazo wanafunzi wa kiume walikuwa wamefanyiwa ukatili wa kingono ambao una madhara makubwa kiafya na kisaikolojia kitu ambacho kinawapelekea kushuka kimasomo.

 

Anasema alipofika shuleni hapo alikutana na kesi za wanafunzi kulawitiwa huko katika familia zao lakini alishindwa kuwabaini kwa kuwa wengi walikuwa wakiogopa kutoa taarifa kwa uongozi na hivyo walijikuta kuwa wanyonge wakati wote, huku wakiendelea kuathirika kimya kimya.

 

Hata hivyo anasema mradi wa ‘Father On Duty’ au ‘Baba wa Zamu’ ambao umeanzisha  mfumo unaoitwa 'Maabara ya Watoto' umeweza kubaini Watoto wa kiume walioathiriwa na vitendo vya ulawiti, wahusika wa vitendo hivyo na umeweza kuwachukulia hatua za kisheria wote waliotajwa kuwafanyia Watoto hao vitendo hivyo ya kikatili.

Baba wa Zamu

 

Anasema pia watoto ambao wamekuwa wakinyanyaswa majumbani aidha kwa kupigwa na wazazi au walezi au kutendewa vitendo vya kikatili vya namna yoyote ile wamekuwa wakiripoti matukio hayo shuleni hapo na hatua zimekuwa zikichukuliwa.

 

Mwalimu Mamboli anasema 'Maabara ya Watoto'  imekuwa ikiendeshwa na 'Baba wa Zamu' ambaye amekuwa  akikutana na mtoto mmoja baada ya mwingine na kuzungumza nae kirafiki zaidi ili kubaini matendo ya kikatili ambayo wamekuwa wakikutana nayo mtaani.

 

"Kwa kweli 'Baba wa Zamu' ameweza kubaini vitendo vingi vya unyanyasaji wanavyofanyiwa Watoto, sisi walimu tulikwama kwa kwasababu wanafunzi wamekuwa wakiogopa kutueleza kutokana na hofu ya  pengine watachapwa lakini wamemueleza Baba wa Zamu' kila kitu.  Na hapa ndipo tulipobaini hali halisi ya ukatili dhidi ya Watoto iliyopo shuleni kwetu,"

 

Anasema katika shule yake kupitia maabara ya Watoto', kumeundwa kikundi Cha Watoto wa kiume 30 ambao miongoni mwao wapo wale wote walioathirika na vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili wa Kingono kwa waliolawitiwa na wengine walionyanyasika kwa namna moja ama nyingine na jamii.

 

Mwalimu Mamboli anasema kupitia maabara hiyo mbali ya  Watoto kuweka wazi vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa pia wamekuwa wakifundishwa aina ya vitendo vya kikatili, namna ya kuepuka navyo na namna ya kuwaripoti wote wanaofanya vitendo hivyo.

 

"Hivi sasa wanafunzi wangu wamebadilika sana, wamekuwa wakija kuripoti mambo ya ajabu yanayoendelea huko mtaani, na kama Kuna mwanafunzi anafanya au amefanyiwa vitendo vya ajabu wanatoa taarifa, hii imekuwa ikitusaidia kupinga vitendo hivi viovu," anasema Mwalimu Mamboli.

 

Anasema sababu mojawapo ya watoto kujikuta wakilawitiwa ni ugumu wa maisha ya wazazi wa mtoto na kusababisha mtoto kushinda na njaa, hivyo anapokutana na watu wabaya huwashawishi kwa kuwapa pesa kidogo na kuwafanyia kitendo hicho cha kikatili.

 

Mwalimu Mamboli anasema yeye binafsi amekuwa akisaidia Wanafunzi waliojikuta wamelawitiwa kutokana na ushawishi wa pesa kwa kuwapatia nafasi ya kula chakula bure shuleni pamoja na kuwanunulia vifaa vya shule ili kuwaepusha na kadhia wanayokutana nayo mtaani.

 

"Unajua tumebaini kuwa sababu kubwa ya Watoto kufanyiwa ukatili wa Kingono ni umaskini wa baadhi ya familia, unakuta mtoto anashinda njaa bila ya kula chochote, shuleni hapati chakula kwa kuwa mzazi hajalipa, sasa akitokea mtu mmoja na fedha zake akamshawishi basi mtoto anajikuta kaingia kwenye mtego, "anasema.

 

Anasema pia Wazazi wamekuwa wakisababisha Watoto wao  kufanyiwa vitendo hivyo kutokana na wengi wao kuishi maisha ya malezi ya upande mmoja (Single Mother), na hivyo wakati mwingi kujikuta wakiwa kwenye mizunguko ya kutafuta fedha huku mtoto akikosa malezi sahihi.

 

" Unakuta Mama yuko sokoni tangu asubuhi mtoto anarudi nyumbani anaendelea kucheza kwenye makundi ya ajabu ajabu  huko mtaani wakati mwingine anakuwa na njaa, Mama akirudi usiku ndio akutane na mtoto wake, sasa huu muda wote lolote linaweza kutokea na huku nyuma mtoto anakuwa hana ulinzi wowote," anasema Mwalimu Mamboli.

 

Daktari Wilson Nyiti ni 'Baba wa Zamu' maarufu kama 'Father on duty' anayesimamia Kata ya Kiranyi ambayo ni miongoni mwa Kata sita zilizopo kwenye mradi huo chini ya shirika la CWCD kusaidia kutoa elimu ya ukatili kwa Watoto na kubaini vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa Watoto katika Kata hiyo ambaye anasema hali ni mbaya.

 

Hata hivyo anasema kupitia mradi huo wameweza kuzuia madhara ambayo bila jitihada za haraka na nguvu ya ziada yangeweza kuendelea kutokea hususani vitendo vya Watoto wa kiume kulawitiwa.

 

Anasema alipopewa jukumu la kusaidia kubainisha vitendo hivyo mashuleni, alijiuliza maswali mengi ya namna atakavyofanikisha utekelezaji wake lakini kutokana na uzoefu na umri mkubwa aliokuwa nao aliweza kukaa na wanafunzi hao ambao walifunguka kwa kumweleza mambo mengi.

 

"Watoto walinieleza mambo makubwa sana, kazi kubwa tuliyoifanya ni kuwapatia ushauri wa athari ya hivyo vitendo na pia tumetoa taarifa kwenye shirika la CWCD ambao na wenyewe wamekuwa wakiripoti Polisi na wahusika wanaofanya ukatili huo kukamatwa,"amesema.

 

Anasema pia wamekuwa wakiwafundisha watoto majukumu ya Baba wa familia na kuwajenga kisaikolojia kuwa wato ni wazazi watarajiwa na wanapaswa kuwa na watoto na kikubwa kuwa walinzi wa familia hivyo kama watafanyiwa vitendo vya kikatili kwa umri waliokuwa nao watapoteza nafasi hiyo.

 

“Pia tumekuwa tukiwafundisha maandiko ya Mungu yanasemaje kuhusu nafasi ya mwanaume katika familia, lakini pia tumekuwa tukiwafundisha elimu ya ujasiriamali kama kilimo n.k, “anasema Dkt Nyiti.

 

Hata hivyo anaiomba Serikali kuweka mkazo kwa watuhumiwa kuweza kufuatiliwa kwa karibu pindi wanapokamatwa na kushtakiwa kwa kuwa kesi nyingi huishia njiani na watuhumiwa kutochukuliwa hatua jambo ambalo linafanya matukio kama hayo kuendelea kushamiri mitaani.

 

Kwa upande wake Mwalimu Mamboli anaiomba Serikali kuongeza ruzuku kwa shule hususani kwenye suala la chakula ili watoto wote waweze kula bure shuleni ili kuwaepusha na vishawishi vya pesa kutokana na njaa wanazokuwa nazo.

 

Akizungumzia Mradi wa ‘Father On Duty’ Mratibu wa mradi huo kutoka taasisi ya CWCD, Epifania Josephat anasema  mradi huo ambao umefadhiliwa na asasi ya Foundation For Civil Society (FCS), umetoa matokeo makubwa lakini pia umepokelewa kwa furaha kubwa na Halmashauri ya Arusha.

 

“Mafanikio ya mradi ni makubwa sana, Halmashauri imepokea kwa furaha na kwa kuwa bajeti yetu ya kuendesha mradi ilikuwa ni kata sita pekee,lakini Serikali ndani ya Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru imeelekeza kata zote zianzishe mradi huo wa ‘Baba wa Zamu’ na tayari wameanza,”anasema.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Dkt Ojung’u Salekwa anakiri vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume umeshamiri sana wilayani Arumeru na kusema mradi wa ‘Baba wa Zamu’ ni mkombozi mkubwa kwa Halmashauri yake.

 

“Mimi niliposikia habari za mradi huu kweli nilifurahi sana, niliupokea kwa mikono miwili na niliufikisha kwenye baraza la madiwani na kukubaliana kuunganisha nguvu kwa kuwa hii ni vita ya pamoja, kwa hiyo mradi huu umeshasambaa wilaya nzima, lengo ni kupambana na vitendo hivi hatari kwa watoto wetu,”anasema.

 

Amesema Serikali wilayani kwake inataka watoto wote walioko shuleni wapewe elimu ya ukatili na kuishauri Wizara ya Elimu kuanzisha mtaala wa somo la ukatili mashuleni na kwamba itapendeza pia elimu hiyo ikashushwa hadi kwenye nyuma za ibada, kanisani na msikitini.

 

Dkt Ojung’u anatoa wito kwa familia kuwa makini na ndugu wa karibu hasa wageni wanapowatembelea kwa kuwa watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ulawiti na ndugu wa karibu wakiamini hawataweza kuwakatili watoto wao kumbe ni tofauti.

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post