Waandishi wa Habari 200 kupimwa afya ya macho Arusha

Dkt Mrisho Mwacha akimpima Uoni Mwandishi Mwanaidi Bundala

 

Na Seif Mangwangi, Arusha

KLINIKI ya macho ya Vision Care imeanza zoezi la kupima Macho Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha ikiwa ni Kuelekea kwenye kilele Cha siku ya Uoni Duniani itakayoadhimishwa Oktoba 12,2023.


Akizungumza wakati wa kuanza zoezi hilo, Mratibu wa zoezi hilo Dkt. Mrisho Mwacha amesema Waandishi wa Habari ni watu muhimu katika nchi hivyo Vision Care imeona ni vyema ikatoa ofa ya Bure kupima Macho Waandishi wa Habari.


Dkt Mwacha amesema kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, zaidi ya Waandishi wa Habari 200 wanatarajiwa kupimwa macho na kupewa ushauri na kuhakikisha wanatekeleza vyema majukumu yao ya kila siku.


Amesema kauli mbiu ya siku ya Uoni Duniani ni " Love your eyes at work", "Penda Macho yako Kazini", na Waandishi wa Habari ni wahanga wakubwa ambao wamekuwa wakitumia sana kompyuta na Simu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kujua afya zao za macho.

Waandishi wa Habari kutoka kushoto, Cynthia Mwilolezi-, Vero Mheta na Zulfa Mfinanga wakiwa wamevaa Miwani baada ya kupimwa na kugundulika kuwa na tatizo la uoni


" Kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha na katika Kuelekea kwenye kilele Cha siku ya Uoni Duniani, leo 10 Septemba, 2023 tumeanza zoezi la kupima Macho Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha na tunatarajia waandishi wa habari 200 watashiriki zoezi hili,"Amesema.


Amesema huduma zitakazotolewa ni pamoja na kupima macho, kutoa dawa na Miwani, kupima presha ya macho, kutoa ushauri kuhusu afya ya macho na  baada ya tatizo kugundulika gharama zitatozwa kwa bei ya chini tofauti na gharama halisi.

Mwandishi Mwanaidi Bundala akipata matibabu


Dkt Mwacha amesema tatizo la macho limekuwa likiongezeka miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu nyingi ikiwemo kukua kwa Teknolojia hususani matumizi ya Tv, Kompyuta na Simu na Waandishi wa Habari ndio watumiaji wakubwa hivyo ametoa wito Kwa waandishi kufika kwa wingi ili kujua afya zao.


" Unajua siku hizi Teknolojia imekuwa sana, matumizi ya vyombo vya kielekroniki ni makubwa, tatizo la macho ni kama magonjwa mengine, huwezi kujua mpaka upate vipimo, unaweza kujiona mzima lakini ukija hapa tukagundua una tatizo kubwa ambalo hukuweza kuligundua ,"amesema.


Mwandishi wa habari John Mhala akipimwa Uoni, kulia ni Dkt Mrisho Mwacha

Amesema watu ambao wamefikisha umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea wamekuwa wakisumbuliwa na presha ya macho na kutoa wito kwa watu kupenda kutumia vyakula vya asili hususani mboga mboga kama karoti na kupunguza kula vyakula vya madukani.


Dkt Mrisho Mwacha akimuhudumia John Mhala 

Aidha ametoa wito Kwa watu wanaotumia Miwani za kununua mtaani kuacha mara Moja na kama ni lazima ni vyema wakafika hospitali kupima Miwani hizo ili waweze kupewa Miwani sahihi kulingana na afya atakayokutwa nayo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post