ZIARA YA UWT KITUO CHA AGAPE YABAINI CHANGAMOTO, NHEMANILO AWAAGIZA MADIWANI VITI MAALUMU KUTAFUTA UFUMBUZI WA HARAKA.

Na Mapuli Misalaba -Shinyanga.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM U.W.T  Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi Rehema Nhemanilo amewaagiza Madiwani wanawake wa kata na  viti Maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kutafuta ufumbuzi wa Changamoto zilizopo katika kituo cha makazi  salama ya  wasichana wahanga wa ukatili ,ndoa na mimba za utotoni  kinachomilikiwa na shirika la Agape  Aids Control  program katika Manispaa ya Shinyanga.

Nhemanilo ametoa agizo hilo leo wakati Wajumbe wa kamati ya utekelezaji  ya Umoja wa Wanawake wa CCM U.W.T  Wilaya ya Shinyanga Mjini  walipotembelea katika kituo hicho kilichopo katika kata ya Chibe Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya U.W.T , ambapo Wilaya ya Shinyanga Mjini imeadhimisha kwa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii ikiwemo kupanda miti na kutembelea wahitaji

Baada ya kutembelea  kituo cha makazi  salama ya  wasichana wahanga wa ukatili ,ndoa na mimba za utotoni  Wajumbe hao wa kamati ya Utekelezaji wakiongozwa na Mwenyekiti Rehema Nhemanilo wamebaini kuwepo kwa changamoto mbali mbali ikiwemo upungufu wa Chakula,Bima za Afya kwa watoto,upungufu wa miundo mbinu ya hostel na Madarasa,Deni la Maji  wanalodaiwa na SHUWASA  la shilingi Milioni 6.3.

Nhemanilo amewataka madiwani hao kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo ambazo zimekuwa kikwazo katika ustawi wa kituo hicho cha watoto wa kike wahanga wa ukatili ,ndoa na mimba za utotoni  kinachomilikiwa na shirika la Agape  Aids Control  program katika Manispaa ya Shinyanga.

“ nawaagiza Madiwani wanawake wa kata na  viti Maalumu  chukueni hatua za haraka kufuatilia na kupata ufumbuzi wa Changamoto zinazokikabili kituo cha Agape, ili Watoto hawa waendelee kupata huduma zote muhimu”

Awali akizungumza na watoto hao wa kike Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Diwani wa kata ya Ndala Mheshimiwa Zamda Shaaban amewaasa wasichana hao kuwekeza zaidi kwenye Elimu ili waweze kukabiliana na soko la elimu na ajira

Katika risala yao watoto hao wa Agape knowledge Open School pamoja na kubainisha mafanikio mbali mbali yaliyofikiwa na kituo hicho cha makazi salama ya  wasichana wahanga wa ukatili ,ndoa na mimba za utotoni ,wametaja changamoto kadhaa ambazo zinahitaji juhudi za pamoja kuzipatia ufumbuzi,ambapo wameomba wadau ikiwemo U.W.T kusaidia msaada wa chakula kwa kuwa sirika halina ufadhili wowote na kwamba halipati ruzuku kutoka serikalini.

Changamoto nyingine kubwa waliyoibainisha kupitia risala hiyo ni deni la shilingi Milioni 6.3 wanalodaiwa na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga SHUWASA ( la kuunganishiwa huduma ya Maji) ambalo limesababisha kusitishiwa huduma ya maji na kufikishwa Mahakamani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha makazi  salama ya  wasichana wahanga wa ukatili ,ndoa na mimba za utotoni  cha Agape  Aids Control  program Bwana John Myola amewaomba wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya umoja wa wanawake wa CCM U.W.T  Wilaya ya Shinyanga Mjini kusaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo katika kituo hicho  ikiwemo deni kubwa la Shilingi Milioni 6.3 wanalodaiwa na SHUWASA.

Bwana Myola amebainisha kuwa takribani Watoto 4,300 wamepata malezi na elimu ya ufundi katika vyuo vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya wananchi  FDC, AGAPE Training centre na SHYNET

Ameeleza zaidi kuwa watoto wapatao 327 wamefanikiwa kupata elimu ya sekondari kupitia shule ya Agape knowledge Open School ali inayowapa nafasi ya kuingia kwenye soko la ushindani wa elimu na ajira,huku watoto 27 wamefanikiwa kujiunga na vyuo vikuu vya Tanzania katika fani mbalimbali.

Madiwani wa viti maalumu Zuhura Waziri na Esther Makune,pamoja na Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi Juliana Buzuruga wametumia nafasi hiyo kuwahamasisha vijana hao wa kike kutumia nafasi hiyo kuweka  bidii,juhudi na maarifa katika masomo ili waweze kuwa kielelezo na mfano thabiti wa ushindi dhidi ya  changamoto walizokutana nazo.

Katibu wa U.W.T Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi Sharifa Hassan Mdee ameeleza malengo ya ziara hiyo kuwa ni kuadhimisha wiki ya U.W.T ngazi ya Wilaya ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe wa kamati ya Utekelezaji U.W.T Wilaya ya Shinyanga Mjini wameshiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo kufanya usafi wa mazingira katika baadhi ya taasisi za Umma, kupanda miti na kufanya usafi katika eneo la ujenzi wa nyumba ya katibu wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini iliyopo katika kata ya kitangili

Wajumbe hao wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini ambao pia walijumuika na Madiwani wa viti Maalumu wakiongozwa na Mwenyekiti Rehema Nhamanilo, wametoa msaada wa vitu mbali mbali kwa watoto hao ikiwemo taulo za kike,juice,sabuni za  Mche na Unga na mafuta ya kupaka.Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga mjini Rehema Nhamanilo akisalimiana na viongozi baada ya kuwasili katika kata ya Kitangili ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya umoja wa wanawake wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.
















This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post