MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA MHE. JOHARI SAMIZI AITAKA JAMII KUWA NA MAADILI MEMA AIPONGEZA KAMPENI YA KUPINGA UKATILI SMAUJATA SHINYANGA.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

   Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amesema ili kutokomeza vitendo vya ukatili ni vyema jamii kuwa na maadili mema na kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

Ameyasema hayo kwenye kikao cha pamoja na viongozi wa kampeni ya kupinga ukatili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga pamoja na mambo mengine suala la utandawazi jamii imekumbushwa kuwa na mipaka katika matumizi ya simu.

DC Samizi amesema mmomonyoko wa maadili katika jamii ni moja ya chanzo cha ukatili hivyo ameitaka jamii kutoa ushirikiano katika kupambana na baadhi ya watu wanaokwenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mkuu  wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amewapongeza viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwa juhudi wanazozifanya katika kuibua na kupambana na ukatili unaoendelea kufanyika kwenye jamii.

Kaimu afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Prisla Mushi amewasisitiza  viongozi wa SMAUJATA kuendelea kuibua ukatili unaofichwa ikiwemo ubakaji, mimba na ndoa za utotoni huku akiiomba jamii kutoa ushirikiano.

Baadhi ya viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga akiwemo katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Daniel Kapaya pamoja na Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Solomon Nalinga Najulwa (Cheupe) wamesema kampeni hiyo itaendelea kuibua na kupambana na ukatili katika jamii.

Aidha viongozi hao wamesema mwanzoni mwa Mwezi ujao Disemba Mwaka huu 2023 katibu wa kampeni hiyo kanda ya ziwa anatarajia kufanya ziara Mkoani Shinyanga hivyo wamesema ziara hiyo itawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na kwamba watatembelea maeneo mbalimbali kutoa elimu ya ukatili.

Shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) ni kampeni huru ya kupinga ukatili Nchini, kauli mbiu yake inasema ‘KATAA UKATILI WEWE NI SHUJAA’ kampeni hiyo inatekeleza majukumu yake chini ya wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum inayoongozwa na Dkt. Dorothy Gwajima.

Mwenyekiti wa SMAUJATA idara ya michezo Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Polisi wa kata ya Ndala Alkwin Willa upande wa kulia akimwonesha cheti cha pongeza cha SMAAUJATA Mkoa wa Shinyanga, mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga pamoja na  kaimu afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Prisla Mushi baada ya kikao leo Jumatatu Novemba 27,2023.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post