MCHANGO WA WANAWAKE KUTOKOMEZA UJANGILI USHOROBA WA KWAKUCHINJA

Na Zulfa Mfinanga, APC Blog

Arusha.

Janeth Sanga, askari uhifadhi wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) ambaye amekuwa mstari wa mbele kukabiliana na uharibifu wa ushoroba wa Kwakuchinja. (Picha na Baraka Ndoto) 
 

Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zilizoridhia mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN Council) mwaka 1979.

Mkataba huu umewapa haki Wanawake kushiriki shughuli mbalimbali ambazo awali zilionekana zinawafaa Wanaume pekee kama vile kupiga kura, kupata elimu, afya pamoja na ajira.

Kufuatia mkataba huo, mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania yamechukua hatua zote zinazofaa ikiwa ni pamoja na kutunga sera na sheria ili wanawake waweze kufurahia haki zao za msingi na uhuru wa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Janeth Sanga (36), Askari wa Wanyamapori wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) iliyopo Wilaya ya Babati Mkoani Manyara ni moja ya matokeo chanya ya mkataba huo hapa nchini.

Janeth ambae ni Mke na Mama wa Watoto watatu ni miongoni mwa wanawake saba waliopo katika kikosi kazi cha askari 40 wa uhifadhi wa Burunge WMA inayolinda na kuendeleza viumbe pori katika ushoroba wa Kwakuchinja.

Ushoroba wa Kwakuchinja ni sehemu muhimu ya makazi na mapitio ya Wanyamapori kati ya hifadhi mbili za Taifa za Tarangire na Ziwa Manyara.

Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise anasema ushoroba wa Kwakuchinja wenye kilomita za mraba 283 ni miongoni mwa shoroba nchini Tanzania ambazo zimeharibiwa zaidi na shughuli za binadamu ikiwemo ukataji wa miti na uwindaji haramu wa viumbepori.

“Changamoto zinazoikabili Burunge WMA ni pamoja na ujangili hasa ujangili wa kitoweo, migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, ongezeko la makazi ya watu na shughuli za kibinadamu, mimea vamizi pamoja na miundombinu ya barabara kuathiri mapitio ya Wanyama,” anasema Mwaise.

 

Wafugaji kuingiza mifugo yao ndani ya Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge imekuwa changamoto katika uhifadhi wa ushoroba wa Kwakuchinja. Hali hii imekuwa ikichangia migogoro kati ya wafugaji na askari wa uhifadhi wanyamapori. (Picha na Zulfa Mfinanga)

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania ina jumla ya shoroba 61 ambapo 41 zipo hatarini kutoweka kutokana na kuvamiwa na shughuli za kibinadamu huku shoroba 20 kati ya hizo zikiwa zimezibwa kabisa.

 

Kuanzishwa kwa Burunge WMA mwaka 2005 ndio ikawa mwanzo wa kurejeshwa kwa maeneo yaliyoharibiwa, kazi ambayo inafanyika mpaka sasa.

Janeth pamoja na askari wenzake wamekuwa wakifanya doria, misako na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa bioanuai katika eneo hilo ili kupunguza uharibifu wa ushoroba huo.

"Doria tunazofanya ndani na nje ya hifadhi zinalenga kudhibiti ujangili wa wanyama na mimea unaosababisha uharibifu wa rasilimali za Taifa pamoja na uharibifu wa mazingira, lakini pia kukagua mipaka ya eneo tengefu ili lisivamiwe," anasema Janeth aliyeanza kazi hiyo mwaka 2006.

Umuhimu wa Wanawake katika Jeshi la Uhifadhi

Janeth ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa kambi ya Burunge WMA anasema mbali na kufanya doria za mara kwa mara ndani ya hifadhi lakini jukumu kubwa ni kutoa elimu kwa jamii huasa wanawake wanaozunguka vijiji vya hifadhi hiyo juu ya uhifadhi wa mazingira.

Janeth ni kiungo muhimu kati ya Wanawake na Jumuiya hiyo kwa sababu kundi hilo limekuwa likitengwa katika maamuzi ya masuala yanayohusu uhifadhi wa bioanuai.

“Jambo la kujivunia ni kuona Wanawake wameanza kubadilika kupitia mimi, huwa nawaambia mimi ni Mwanamke kama ninyi, nahitaji nishati kwa ajili ya kupikia, nahitaji fedha kwa ajili ya kuendesha maisha, lakini vyote hivyo havijanifanya nivunje sheria za uhifadhi kwa kukata miti ama kushiriki kwenye biashara ya kuuza ama kununua nyamapori,” anasema Janeth.

Janeth anasema Wanawake wamekuwa wakitumika zaidi kwenye ujangili wa Wanyamapori kwa ajili ya kitoweo kwa kununua na kuuza kupitia biashara ya mama lishe hivyo amekuwa akitembelea minada mbalimbali kwa ajili ya kufanya doria pamoja na kutoa elimu kwa wanawake ili kukomesha biashara hiyo.

Sheria ya Uhifadhi namba 5 ya mwaka 2009  inaelekeza kwamba mtuhumiwa wa kike akamatwe na askari wa kike na mtuhumiwa wa kiume akamatwe na askari wa kiume.

"Kazi hii naipenda ingawa ina changamoto zake kwamba kuna baadhi ya watu hawatupendi lakini hao ni wale wasiopenda kutii sheria za wanyamapori, lakini kwa upande mwingine kazi yangu inaendelea kuivutia jamii," anasema askari huyo.

 

Janeth Sanga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) walipomtembelea katika kambi ya Burunge WMA baada ya mafunzo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. (Picha na Baraka Ndoto).


Janeth Ameacha alama isiyofutika

Janeth anajivunia kuwashawishi Wanawake watano kuingia katika shughuli za uhifadhi kutoka vijiji tofauti.

Anasema wote hao walikuwa wanamuuliza maswali mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo nafasi ya Mwanamke katika uhifadhi hivyo kupitia kwake walishawishika zaidi na walipata sehemu ya kuanzia.

"Kuna dhana kwamba ukiajiriwa huwezi kutimiza majukumu ya familia yako kama Mama, naomba niwatoe hofu, mimi nina zaidi ya miaka 10 kwenye hii kazi lakini familia yangu naihudumia ipasavyo na majukumu ya kazi yanaenda vizuri kabisa," anasema Janeth.

Askari huyo alikuwa akihojiwa hivi karibuni na Mwandishi wa makala haya katika mafunzo ya vitendo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. 

Monica Lugiriza (23) ni miongoni mwa askari watano waliojiunga na Jeshi la Uhifadhi mwaka huu kwa ushawishi wa Janeth licha ya kuwa tangu akiwa mdogo aliipenda kazi hiyo.

“Shauku yangu iliongezeka zaidi baada ya kumuona Janeth, na nikiri kwamba hadi kufikia hapa leo kuna mchango wake mkubwa,” anasema Monica.

Monica anasema kile ambacho alikuwa akiwaza kabla ya kujiunga na jeshi hilo ndicho alichokutana nacho ambacho ni kutoa elimu ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii na kulinda maeneo tengefu.

Familia na jamii yake inaendelea kumpa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii.

Kikosi kazi cha askari wa uhifadhi kimekuwa nguzo muhimu ya kutokomeza ujangili na kuufanya ushoroba wa Kwakuchinja kuanza kuwa kivutio cha wanyamapori na watalii. (Picha na Baraka Ndoto).

Askari wanawake wanavyotambuliwa katika uhifadhi

Kikosi kazi cha kukabiliana na ujangili chenye askari 40 kimeundwa na taasisi nne za Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), shirika lisilo kuwa la Serikali la Chem Chem Association, Burunge WMA na Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Meneja Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kutoka Chem Chem Association, Martin Mung’ong’o anasema kwa kushirikiana na taasisi hizo nne wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja ya kutoa elimu, kufanya doria na kuhakikisha watuhumiwa wa ujangili wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

Mung’ong’o anasema mafanikio ya kikosi kazi hicho yamechangiwa na askari wanawake akiwemo Janeth ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri hasa kuwabaini na kuwakamata wanawake wanaojihusisha na ujangili.

"Wateja wakubwa wa biashara ya nyamapori ni wanawake wa majumbani pamoja na Mama lishe. Kuwatumia askari wetu hususani askari wanawake tumefanikiwa kuwatia nguvuni baadhi ya wanunuzi na wauzaji, na hadi sasa biashara hii inaendelea kukoma kabisa," anasema Mung’ong’o. 

Mahema yanayotumiwa na askari na wanyamapori wa Burunge WMA katika moja ya kambi zao wanazotumia kupanga mikakati ya namna ya kukabiliana na majangili.  (Picha na Baraka Ndoto)

Sera ya Wanyamapori ya Tanzania ya mwaka 2007 inaitaka Serikali na wadau wa uhifadhi kulinda shoroba za wanyamapori, njia za uhamaji, maeneo ya usalama wa wanyama, na kuhakikisha kwamba jamii zilizo katika maeneo hayo ya wanyama zinafaidika vilivyo kutokana na uhifadhi wanyamapori.

Mtaalamu wa masuala ya bioanuai na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Angelmercy Baltazary anasema lengo la kuhamasisha wanawake wengi kuingia katika uhifadhi ni kuweka usawa wa jinsi zote kushiriki katika utunzaji wa bioanuia.

"Makundi yote kwa maana ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wana mchango mkubwa sana katika utunzaji wa mazingira kwani wasiposhirikishwa itasababisha kukosa haki juu ya ardhi yao ikiwemo uwakilishi mdogo katika maamuzi ya maliasili na uongozi," anasema mtaalam huyo.

Angelmercy aliyekuwa akizungumza katika mafunzo ya siku tatu ya kuripoti habari za bioanuai kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Afrika chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili anasema  wanawake washirikishwe katika ngazi zote za maamuzi ili kutoa mchango utakaosaidia kuimarisha shughuli za uhifadhi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoingia na zinazotekeleza Mkataba wa Lusaka wa kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyama na mimea ndani na nje ya bara hilo (Lusaka Agreement Task Force-LATF) ulioanzishwa mwaka 1994.

Kufuatia mkataba huo, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa uhifadhi wa rasilimali za misitu na wanyamapori kwa kuimarisha ulinzi na nidhamu kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuanzisha Jeshi Usu la Uhifadhi (JU) mwaka 2018.

Ramani inanyoonyesha eneo la hifadhi ya Burunge WMA pamoja na maeneo ambayo imepakana nayo (Picha kwa hisani ya Google earth)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki aliyekuwa akizungumza katika Kongamano la kwanza  la kitaifa la kujadili usimamizi wa shoroba Disemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam alisema wizara yake itaendelea kushirikisha wadau na makundi mbalimbali kwenye jamii ili kuokoa shoroba zisiharibiwe. 


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post