MKOA WA SHINYANGA WAZINDUA KAMPENI YA ONGEA NAO KAMANDA MAGOMI ATOA TAKWIMU ZA UKATILI WA KIJINSIA.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amesema mpaka sasa kesi za ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa Mwaka huu 2023 ni kesi 105 ambapo Mwaka jana jumla ya kesi 97 ziliripotiwa Mkoani Shinyanga.

Ametoa takwimu hizo kwenye  uzinduzi wa kampeni ya Ongea nao Mkoa wa Shinyanga iliyokwenda sanjari na siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo hafla hiyo  imefanyika  katika viwanja vya shule ya msingi Buduhe Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Kamanda Magomi amesema kuongezeka kwa kesi za ukatili wa kijinsia Mkoani Shinyanga ni kutokana na elimu inayoendelea kutolewa kwa wananchi katika kuripoti kesi za ukatili huku akiwasisitiza wananchi kutofumbia macho kesi za ukatili wa kijinsia zinazoendelea kufanyika kwenye familia ama jamii wanayoishi.

Hata hivyo Kamanda Magomi ametumia nafasi hiyo kuwataka wanafunzi, wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto.

‘Tunawataka wanafunzi, wananchi na wadau kutambua kuwa mnawajibika na kupaza sauti na kutoa taarifa za uhalifu katika vyombo vya sheria ili kutokomeza vitendo hivyo katika jamii inayotuzunguka kwani jukumu la ulinzi na usalama nila kila mwananchi hata hivyo ni vyema mkatambua kuwa ukatili wa kijinsia ni changamoto kubwa katika jamii na wahanga wakubwa ni watoto na wanawake hivyo hamna budi kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa wakati ili wahalifu waweze kukamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria’.amesema kamanda Magomi

Kamanda magomi ametaja matendo ya ukatili wa kijinsia kuwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti, kipigo, kutelekeza familia, kutumikisha watoto na kuwazorotesha masomo, lugha za matusi na ndoa za utotoni.

Amesema madhara ya ukatili wa kijinsia ni pamoja na vifo, mimba za utotoni, maradhi yanayosababishwa na ngono mfano UKIMWI, ulemevu wa kudumu, kuongezeka kwa watoto mtaani, umaskini, msongo wa mawazo na mmomonyoko wa kifamilia.

Pia amewataka wananchi kutambua mifumo mbalimbali ya utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia mifumo hiyo ni pamoja na dawati la jinsia na watoto Polisi, viongozi wa Dini, ustawi wa jamii, viongozi wa serikali za mitaa au mtu yoyote anayeaminika kwenye jamii hiyo.

Kamanda Magomi ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuungana kwa pamoja katika kampeni ya Ongea nao hususan kwenye masuala ya kutoa elimu kwa wananchi wa lika zote ili Mkoa wa Shinyanga uendelee kuwa salama.

Akizungumza mgeni rasmi katika hafla hiyo, katibu tawala wa Wilaya ya kishapu Bi. Fatma Mohamed pamoja na mambo mengine amewakumbusha wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na serikali katika kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

Baadhi ya wadau mbalimbali wa kupambana na ukatili akiwemo mwakilishi kutoka kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga pamoja na mwakilishi kutoka kampeni ya sauti ya watoto Tanzania wamesema wataendelea kuibua na kutokomeza ukatili unaoendelea katika familia na jamii kwa ujumla.

Mtandao wa Polisi wanawake Tanzania (TPF - NET) Mkoa wa Shinyanga leo Disemba 1,2023 umezindua  kampeni ya Ongea nao ambayo inatekelezwa na Polisi wanawake Mkoa wa Shinyanga ambapo mwenyekiti wa mtandao huo Mkoa wa Shinyanga ni RPC Janeth Magomi. 

Kauli mbiu yake inasema “Wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia” na ‘Polisi jamii kwa usalama na maendeleo yetu” ambapo lengo lake ni kutoa elimu kwa vijana, wazee, watoto kuhusu masuala ya usalama wa raia na mali zao, ukatili wa kijinsia, mauaji pamoja na mmomonyoko wa maadili. 

Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-NET) Mkoa wa Shinyanga baada ya kuzindua kampeni ya "ONGEA NAO" umegawa  taulo za kike na madaftari kwa wanafunzi, kutoa mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji kaya 50 katika kata tatu za Wilaya ya Kishapu,kutoa msaada wa kilo 250 za mchele, Sabuni miche 50, Sukari kilo 100, Maharage kilo 100 na mafuta ya kupikia kilo 50.  

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi ambaye pia ni mwenyekiti wa TPF – NET Mkoa wa Shinyanga akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Ongea nao Mkoa wa Shinyanga iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Buduhe Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Mgeni rasmi, katibu tawala wa Wilaya ya kishapu Bi. Fatma Mohamed akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Ongea nao Mkoa wa Shinyanga iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Buduhe Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.



Mgeni rasmi, katibu tawala wa Wilaya ya Kishapu Bi. Fatma Mohamed akiendelea na zoezi la kugawa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo  taulo za kike na madaftari kwa wanafunzi, mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji kaya 50 katika kata tatu za Wilaya ya Kishapu.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post