Na Mapuli Kitina Misalaba
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga leo Alhamis Februari 8,2024 limepitisha
mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kiasi cha Shilingi
Bilioni 40.5
Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe Ngassa Mboje baada ya Madiwani kurithia kwa
pamoja kwenye mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kupokea, kujadili na
kupitisha rasimu ya mpango na bajeti 2024/2025 ambao umefanyika katika ukumbi
wa makao makuu ya Halmashauri hiyo.
Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti huyo
ametamka rasmi kuridhia bajeti hiyo yenye jumla ya Bilioni 40.5 huku
akisisitiza changamoto zilizopo kutatuliwa haraka ikiwemo ya ukusanyaji wa
mapato ya ndani ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Mmetuonyesha
nini tunatarajia kukifanya katika Mwaka wa Fedha unaokuja katika mapendekezo
yenu wataalam wetu lakini sisi tumeridhia kwa pamoja na waheshimiwa Madiwani
wajumbe wa Baraza maalum kupitisha bajeti yenye jumla ya Shilingi Bilioni 40.5
tunashukuru sana lakini kuna mambo ambayo tumeelekeza yafanyiwe kazi lakini
kubwa sana ikiwa ni kiashiria cha hatali lile la Miezi sita (6) nusu Mwaka kuwa
na asilimia 32 hiyo tuichukulie kama kiashiria cha hatali tunakwenda kumalizaje
Mwaka wa Fedha unaoendelea sisi kama wawakilishi wa wananchi nia yetu ni
kuhakikisha kwamba tunawahudumia wananchi wetu ambao wametuchagua katika yale
ambayo wanayahitaji”.amesema
Mhe. Mboje
Kutokana na hali ya ukusanyaji wa mapato
ya ndani katika Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Shinyanga ambapo kwa Miezi sita
ya Mwaka huu wa Fedha 2023/2024 umefikia asilimia 32 mpaka sasa.
Baadhi ya Madiwani kutoka kata
mbalimbali za Halmashauri hiyo wamemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia malengo
waliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kuongeza vyanzo vya mapato ambavyo
vimesahaulika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo Kisena Mabuba pamoja na mambo mengine ameahidi kushughulikia changamoto
hiyo huku akiwaomba Madiwani kuendelea kusimamia mapato.
“Niombe
sasa tuanze upya sisi tuwe kitu kimoja wakuu wa idara na watumishi wengine wote
na waheshimiwa Madiwani tuzungumze sauti moja tunapomzungumzia mtu anatorosha
ushuru tumzungumzie wote kwa sauti moja kama kuna mtu hawajibiki tumzungumzie
wote kwa sauti moja hilo litatusaidia sana kila mmoja ajue mipaka yake na
tupate kuisimamia tukifanya hivo mimi naomba niwatoe hofu tunatoka hapa tulipo,
kuna watendaji mpaka wapigiwe simu mimi nimeshazungumza nao nimewaambia suala
la mapato siyo suala la kubembelezana ni suala la wajibu kwa kila mtendaji”.amesema Mabuba
Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga vijijini Edward Ngelela amemsihi
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia suala la mapato ya ndani huku
akishauri kuundwa timu maalum kwa ajili ya kufuatilia suala hilo kwa watendaji
wa kata ambapo pia amewaomba viongozi wa Halmashauri hiyo wakiwemo Madiwani
wafanyabiashara kuwa mfano katika suala la kutoa ushuru.
Naye katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga amewakumbusha viongozi wa Halmashauri hiyo kuepukana na rushwa wakati wa utekelezaji
wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwenye mamlaka za kisheria kwa
watu watakaobainika kujihusisha na rushwa.
Kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga Ibrahim Makana amelipongeza
Baraza ma Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa kuridhia na kupitisha mapendekezo ya
mpango wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kiasi cha Shilingi Bilioni 40.5.