TEKNOLOJIA MPYA YA UKAGUZI WA MAGARI KUWAONDOA BARABARANI MADEREVA WASIO NA SIFA

_Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Arusha Profesa Musa Chacha akitoa maelezo juu ya teknolojia mpya kwa Wakuu wa Usalama Barabarani Nchini_

 

Na Egidia Vedasto, Arusha

Chuo cha Ufundi Arusha (ATC ) kwa kushirikiana na jeshi la polisi pamoja na Taasisi ya Mitambo Mizito na Teknolojia (IHET) wameanzisha teknolojia mpya ya kudhibiti ajali za barabarani nchini.

Akizungumza na Wakuu wa Usalama Barabarani na wakaguzi wa magari nchini, Mkuu wa chuo hicho Profesa Musa Chacha amesema wamejipanga kutoa elimu inayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia ya mitambo ya kisasa ya kufundishia.

_Wakuu wa Usalama Barabarani wakifuatilia kwa makini mpango mkakati wa utoaji  mafunzo ya kwa kutumia teknolojia ya kisasa kutoka kwa uongozi wa chuo Cha Ufundi Arusha_

Profesa Chacha amesema elimu inayotolewa katika Chuo hapo ni ya hali ya juu itakayowahakikishia madereva kupata  uelewa na umakini pindi wanapokuwa barabarani.

Aidha amewaomba wasimamizi wa barabarani na wakaguzi wa magari  kutoa elimu ya kutosha kwa madereva ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujiunga kuongeza elimu katika Chuo hicho kinachofanya vizuri Afrika Mashariki ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia yaliyopo sasa.

Profesa Chacha ameongeza kuwa pia chuo hicho kinatoa mafunzo ya saikolojia ya kutambua muda wa dereva kupumzika na kuendesha chombo cha moto, kutoa elimu ya afya na jinsi ya kuwakarimu  wateja ndani ya magari.

"Tunataka madereva wapate elimu sahihi na kufahamu juu ya mabadiliko ya teknolojia yanavyoenda kwa kasi, kwa sasa kuna magari yanayotumia umeme na mengine yanatumia gesi, na tumeshajipanga kimiundombinu na vifaa vya kisasa vya kufundishia na ukikuta ajali imetokea moja kwa moja ujue kuwa dereva hana elimu ya kutosha" amesema Profesa Chacha.

Kwa Upande wake Naibu Kamishna Mwandamizi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Ramadhan Ng'anzi amesema mwezi Machi mwaka huu ukaguzi wa magari utaanza kufanyika kwa kutumia mitambo ya kisasa.

Kamanda Ng'anzi amesema hayo baada ya kufanya ukaguzi katika karakana  zilizopo chuoni na kujiridhisha na hatua hiyo kubwa itakayosaidia wakaguzi kutumia mitambo ya kisasa ya kukagua magari tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma na kusaidia kupunguza ajali za barabarani. 

"Mafunzo haya yatatuondolea dhana iliyozoeleka ya kugalagala uvunguni mwa magari kufanya ukaguzi na badala yake kwenda na teknolojia katika ukaguzi ambayo naamini itapunguza sana ajali za barabarani" ameeleza Ng'anzi.

Hata hivyo ametoa wito kwa madereva wote nchini kujiunga na Chuo cha Ufundi Arusha ili kuongeza maarifa na ujuzi katika kazi zao na kutambua magari   ambayo ni salama kwa sababu teknolojia imekua.

Wakati huohuo Fundi mitambo idara ya mitambo Frank Moshi amesema Chuo hicho pia  kina wataalam wa kutosha wa kutengeneza vifaa tiba ambavyo vimekuwa mchango mkubwa katika baadhi ya hospitali ikiwemo ya Mount Meru iliyopo Arusha  na KCMC iliyopo Moshi.

"Tumekuwa tukitengeneza baiskeli za matairi matatu maarufu kama (wheelchair) vitanda vya hospitalini na miundombinu ya kihifadhia maiti (Cold room), milango isiyotoa hewa na vifaa vingine vingi, kwa hiyo hata katika hospitali yetu inayojengwa hapa chuoni inayotarajiwa  kuanza kutoa huduma mwezi wa June mwaka huu tunategemea kutengeneza wenyewe vifaa tiba kwa asilimia kubwa" amesema Moshi.

_Wakuu wa Usalama Barabarani na wakaguzi wa magari wakiwa katika karakana ya mitambo katika Chuo Cha Ufundi Arusha_
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya waongoza watalii Tanzania Timothy Mdinka amesema, Chuo Cha Ufundi Arusha kimesaidia kuimarisha taaluma ya udereva kwa  waongoza watalii wengi nchini na kuwajengea imani watalii wanaoingia nchini.

"Mkumbuke siku za nyuma watalii walikuwa wakija nchini kutalii walikuwa hawarudi salama makwao lakini kwa sasa baada ya mafunzo waliyopewa madereva yamesaidia kuboresha taaluma zao na kuwajengea imani wageni na kutangaza jina zuri la Tanzania pindi wanaporudi kwao" amesema Mdinka.

Chuo Cha Ufundi Arusha kilianzishwa mwaka 1978 baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Ujerumani ambacho kinatoa elimu hadi ngazi ya udaktari katika Ufundi na kinaongoza barani Afrika kwa kuwa na karakana za kisasa pamoja na wataalam waliobobea katika ufundishaji.

_Jeshi la polisi, Viongozi wa chuo Cha Ufundi Arusha na Wakuu wa chuo Cha Mitambo (IHET) katika picha ya pamoja_

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post