JOWUTA:ASILIMIA 80 YA WAANDISHI HAWANA MIKATABA YA AJIRA

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Waandishi wa Habari nchini (JOWUTA), Mussa Juma akizungumza katika kikao cha tathmini ya sekta Habari kilichofanyika leo Jijini Arusha

 Egidia Vedasto,

Arusha.

Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini (JOWUTA) kimeendelea kuikumbusha serikali kutatua changamoto ya mikataba na ajira kwa waandishi wa habari nchini.

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wadau wa Sekta hiyo, Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma amesema asilimia 80 ya waandishi wa habari nchini hawana mikataba ya ajira.

Juma amesema iwapo serikali itatatua changamoto hiyo ni wazi kuwa serikali itaongeza mapato kutokana na michango ya kodi na mapato kutoka kwa waandishi hao takribani elfu kumi waliopo nchini.

Amesema changamoto ya kukosekana kwa mikataba imesababisha waandishi kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiuchumi hasa pale wanapougua au kuuguliwa.

"Wengi wa waandishi wa habari hawana vipato vinavyoeleweka kwa sababu wanafanya kazi kama za Day worker, hali inayosababisha kuisha maisha ya dhiki" amesema Juma.

Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mtaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani, Juma ameiomba Wizara ya habari kwa kushiriana na wadau wake kuja na sera ambayo itawalinda waandishi wa habari wakati wanapotelekeza majukumu yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Deodatus Balile ameiomba serikali kutoa mtaji katika vyombo vya habari ili kutimiza malengo ya vyombo hivyo pamoja na kukuza uchumi wa nchi. 

Aidha amesema serikali iruhusu uwekezaji utakaosaidia kukuza uchumi wa vyombo vya habari  kama inavyofanyika katika sekta nyingine. 

"Makampuni ya simu yanapata wawekezaji kutoka nje  kwa asilimia 100 lakini kwenye sekta ya habari hata akitokea mwekezaji wa asilimia 51 kutoka nje inashindikana, ifike mahali serikali iruhusu uwekezaji ili kuinua sekta ya habari ambayo pia itasaidia kukuza uchumi wa nchi" amesema Balile

Kwa upande wake Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Sekta zingine umeimarishwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Amesema kutokana na kikao hicho cha Tathmini serikali itazingatia   maazimio yote yaliyozungumzwa na taasisi mbambali na kisha kufanyiwa kazi ili kuboresha huduma katika jamii.

Nnauye ameongeza kuwa, malengo ya Wizara yake ni kufikiwa kwa dira yake ambayo ni kuwa na jamii yenye habari sahihi na iliyowezeshwa kidigitali kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambapo michango ya sekta zote inategemewa.

Katika ufafanuzi wake amewakumbusha TCRA kutafuta namna ya kuboresha huduma za mawasiliano katika ushirika wa miundombinu.

"Inaweza kuwa hivi, laini zote kutumika katika mtandao mmoja kwani wingi wa nguzo za minara ya simu inakuwa kama uchafu, na pia liangaliwe suala la uwiano wa laini za simu milioni 70 kwa watumiaji milioni 61"

"Tangu kuanzishwa kwa Wizara hii ni mwaka sasa, ambapo Rais aliona vema kuunganisha wizara hii na kuwa Wizara ya Habari Mawasiliano  na Teknolojia ya Habari,  tunajivunia mabadiliko hayo, utendaji kazi umerahisishwa na kuimarisha lakini pia huduma ya mawasiliano kwa jamii imesogezwa  sana" amesema Nnauye

Nnauye amefafanua kwamba majadiliano kati ya Wizara yake na Umoja wa Sekta ya watoa huduma ya habari nchini yameleta manufaa ya kuimarika kwa ushirikiano pia kupunguza gharama za uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano.

Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura (wa kwanza kulia) na Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo (wa pili kulia) wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao hicho

Amesema manufaa mengine ni Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, nchi imekuwa miongoni mwa nchi zinazoheshimu faragja za watu na kuongeza idadi ya  watu wenye furaha.

Kikao hicho kimejumuisha washiriki zaidi ya 200, kutoka wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wenyeviti wa vyombo vya habari na wadau wengine  wa sekta mbalimbali huku zaidi ya watu 3000 wakifuatilia kikao hicho kupitia mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imejipanga kupiitisha bajeti ya bilioni 178 katika mwaka wa fedha 2024/2025.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post