Na Seif Mangwangi,
Ruaha
ASKARI wa Jeshi Usu la Uhifadhi katika hifadhi ya Taifa Ruaha Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, wamekamata Ng'ombe 547 na punda3 ikiwa inalishwa ndani ya hifadhi hiyo kinyume Cha Sheria za Uhifadhi huku wamiliki wa mifugo hiyo wakikimbia.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, shirika la hifadhi za Taifa Tanzania na Mkuu wa hifadhi ya Ruaha, Goodwill Meng'ataki amesema mifugo hiyo imekamatwa katika eneo la ukwaheri ndani ya bonde Oevu la Ihefu.
Akizungumza Machi27,2024 katika eneo la Ukwaheri ambapo mifugo hiyo imehifadhiwa baada ya kukamatwa, Meng'ataki amesema eneo hilo ambalo mifugo hiyo imekamatwa ni katikati ya hifadhi ya Ruaha katika bonde la Ihefu mahala ambapo ni chanzo kikuu cha maji ya mto Ruaha mkuu.
Kundi la mifugo 547 na punda 3 wakiondolewa kutoka eneo Oevu la Ihefu baada ya kukamatwa ikilishiwa ndani ya hifadhi hiyo. |
Meng'ataki amesema baada ya kukamatwa kwa mifugo hiyo, walifuata taratibu za kisheria ikiwemo kufikisha suala hilo Polisi na baadae katika Mahakama ya Wilaya ya Mbarali na tayari Mahakama imeshatoa hukumu ya kutaifishwa kwa mifugo hiyo nakuagiza iuzwe.
"Kwa kawaida tunavyokamata mifugo ndani ya hifadhi, tunawasiliana na Polisi na kuifikisha Mahakamani. Tayari Mahakama imetolea maamuzi mifugo iliyokamatwa na imeagiza iuzwe, tunasubiri wanunuzi ambao tayari wako njiani kuja hapa Ukwaheri kwaajili ya kununua,"amesema.
Amesema wafugaji katika bonde la Ihefu katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wamekuwa wabishi kuelewa katazo la kutochungia mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo na wamekuwa wakitumia mwanya wa eneo hilo kuwa na maji mengi kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa na Askari wa Jeshi Usu la Uhifadhi.
"Ni takribani sasa miaka miwili tumekuwa tukitunza eneo Oevu la Ihefu baada ya kuondolewa kwa wafugaji ambao wamekuwa wakiharibu sana eneo hili, tumekuwa tukitumia ndege na Helkopta kuhakikisha tunaondoa mifugo yote, lakini wafugaji wamekuwa wabishi sana, hii ni hatari kwao sababu sisi tunafuata Sheria, tukikamata tunawapeleka mahakamani mifugo, niwasihi tu waache kuingiza mifugo,"amesema na kuongeza:
.. Kipindi hiki Kuna mvua nyingi zinanyesha ukanda huu, hawa wafugaji wamekuwa wakitumia mwanya huo huo kuingiza mifugo yao kwenye maeneo yenye maji mengi wakijua Askari wetu hawawezi kufika huko, lakini tunajitahidi kukabiliana nao,"Amesema.
Amesema changamoto nyingine ni Askari wake kukabiliana na wafugaji ambao wamekuwa wakitumia silaha za jadi ikiwemo mishale na mikuki pindi wanapokamatiwa mifugo yao wakitaka kuitorosha.
Afisa Uhifadhi daraja la pili na Mkuu wa Kanda ya Usangu, Abisai Nassari amesema baada ya kukamata mifugo hiyo 547 na punda 3, walitumia msaada wa helkopta kuisogeza hadi katika eneo lenye maji machache ndipo askari wake wakaisogeza hadi eneo la ukwaheri.
"Tunashukuru Serikali ya Rais Mama Samia kutuletea vifaa vichache vinavyotusaidia kupambana na mifugo na majangili wa wanyamapori, tunaomba kuongezewa vifaa zaidi ili tuweze kufanyakazi yetu kwa ufanisi zaidi,"anasema.
Anasema changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni namna ya kuwakabili wafugaji wanaoingiza mifugo katika bonde la Ihefu kwa kuwa eneo hilo ni chepechepe lililojaa matope kutokana na kuteremsha maji wakati wote.
Kundi mojawapo la ng'ombe likiwa eneo Oevu la Ihefu ndani ya hifadhi ya Ruaha |