Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa akiwa na Waziri wa Ardhi na Makazi, Jerry Slaa katika Moja ya vikao vya kusikiliza kero za Ardhi kwa wakazi wa Arusha |
Na Egidia Vedasto
Arusha.
Wananchi wametakiwa kupata ufafanuzi katika ofisi za viongozi wa mitaa, vijiji na kata kabla ya kununua maeneo ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.
Akizungumza na mwandishi wa APC Blog ofisini kwake leo, Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa amesema baadhi ya viongozi wasio waaminifu wamekuwa wakiuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu kumi hali inayoleta taharuki na kuongeza mnyororo wa migogoro.
Aidha amesema kuwa, kwa kipindi cha wiki moja kuanzia tarehe 19-24 mwezi March mwaka huu, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ametatua kero zaidi ya mia tatu nyingi zikisababishwa na viongozi kuuza maeneo kwa zaidi ya mtu mmoja.
Hata hivyo ameyataka makampuni yote yanayojihusisha na biashara ya kupima na kuuza viwanja kuacha mara moja kuuza bila kuwa na hati ili kuepuka migongano na kuendana na ramani ya Jiji.
"Nawasihi wananchi msiyaamini makampuni hata kidogo kwa sababu hao pia ni chanzo kikubwa cha matatizo, na kesi nyingi zimekuwa zikiripotiwa baada ya wananchi kuuziwa viwanja wanaambiwa kupata hati wanatakiwa wapambane wenyewe jambo ambalo ni kinyume cha sheria" amefafanua Mtahengerwa.
Mtahengerwa amesisitiza kwamba makampuni yanayohusika na kuuza viwanja yamekuwa yakifanya shughuli zake bila kuzingatia utaratibu wa mipango miji inayoonesha wapi kufanyike makazi ya watu na wapi iwe sehemu ya biashara.
Ameongeza kuwa migogoro mingine imekuwa ikitokana na wananchi kuvamia maeneo yaliyotengwa na serikali na kujimilikisha kinyume cha sheria ambapo baada ya muda wananchi huigeukia serikali na kudai wamedhulumiwa.
Mtahengerwa pia, amewakumbusha watu wanaojifanya wana pesa na wako juu ya sheria ambao wamekuwa wakivamia maeneo ya watu na kujenga maghorofa, ikibainika sio haki yao maghorofa yatashushwa chini ili mwenye haki amiliki eneo lake.
"Hakuna mtu mwenye nguvu zaidi ya dola, hata kama umejenga kwa mabilioni ya pesa, kama sio halali yako ujue umekwama na hutaendeleza ujenzi hata kama umefikia hatua za mwisho" amesisitiza Mtahengerwa.