Egidia Vedasto
Arusha
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema, Afrika bado ina mchango mdogo katika ukuaji wa utalii duniani hivyo jitihada kubwa zinahitajika.
Akifungua Kongamano la uwekezaji kwenye Sekta ya Utalii katika Mkoa wa Arusha lililofanyika Jijini Arusha, Mkumbo amesema Bara la Afrika Lina mchango mdogo katika suala zima la ukuaji wa utalii ukilinganisha tofauti na mchango mkubwa wa utalii kutoka Bara la Ulaya.
Aidha, Prof Mkumbo amesema ifikapo Julai 1 mwaka huu atakuwa Arusha kwa ajili ya kufungua kituo Cha uwekezaji, kwa lengo la kuimarisha zaidi sekta ya uwekezaji na kukuza utalii kwa ujumla.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo katika Mkutano wa Wadau wa Utalii Jijini Arusha |
"Katika bara la Afrika tuna mchango mdogo sana katika ukuaji wa Utalii ni kama asilimia ndogo hivyo sekta ya utalii bado tunapaswa kufanya bidii sana ili kukuza utalii duniani" amesema Mkumbo.
Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki amesema bado kuna Kazi kubwa kuhakikisha wanafikia malengo ya ongezeko la watalii kufikia milioni tano Kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, na kwamba huku akisema kuwa umebaki mwaka mmoja ambao ni muda mchache, hivyo kunahitajika Kasi ya juu kufanikisha jambo hilo.
"Bado matamanio yetu ni kufikia malengo ya kupata watalii milioni tano kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na muda wa mwaka mmoja uliobaki ni mchache na ukizingatia mpaka sasa watalii walioingia nchini ni milioni 1.8 hivyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya"amesema Kairuki.
Amesema wako katika harakati ya kuboresha maeneo ya uwekezaji katika utalii hasa katika Miundombinu ya malazi na hoteli pamoja na kituo cha kisasa cha mikutano kinachojengwa na Kituo cha mikutano cha kimataifa cha AICC kinachotarajia kubeba watu 10000 kwa wakati mmoja.
Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi Iman Nkuwi, amesema lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha wawekezaji kwenye Sekta ya Utalii kujadiliana Kwa pamoja namna gani wanakwenda kuboresha na kuimarisha sekta ya Utalii hususani katika suala Zima la uwekezaji wa miundombinu Mbalimbali Katika mkoa wa Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda |
"Nataka Arusha iwe ya dola na sio shilingi, hata muuza mchicha na muendesha bodaboda ajivunie mkoa huu wa utalii, ili hata wageni kutoka nje wakiingia wafurahie mandhari ya Arusha" amesema Makonda.
Kongamano la Uwekezaji wa Utalii Nchini limefanyika jijini Arusha na kuwakutanisha Wadau mbalimbali wa Utalii.
_Wadau mbalimbali katika mkutano wa Sekta ya Uwekezaji na Utalii leo Jijini Arusha |