Biashara mbadala za wanawake zachochea uhifadhi Kwakuchinja

Cecilia Philipo akiwa katika kazi zake za kawaida za kusuka ukili

Na Zulfa Mfinanga, 

Manyara. 

Kwa watumiaji wa barabara kuu inayotoka jijini Arusha hadi Babati Mkoani Manyara ni jambo la kawaida kuwaona akina mama kandokando ya barabara hiyo wakiuza bidhaa za utamaduni. 

Biashara wanazofanya ni pamoja na uuzaji wa bidhaa za mapambo ya mwili na majumbani zilizotengenezwa kwa kutumia malighafi za asili zinazowavutia zaidi watalii wanao tembelea vivutio vilivyopo ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja kwa ajili ya kujionea wanyamapori. 

Ushoroba wa Kwakuchinja ni mapitio na makazi ya asili ya wanyamapori yanayounganisha hifadhi mbili za Taifa za Tarangire na Ziwa Manyara unaopatikana katika mikoa ya Arusha na Manyara. 

Akina mama hao hupatikana zaidi vijiji vya Minjingu na Vilima vitatu vyote vikiwa kata ya Nkaiti, wilaya ya Babati katika mkoa wa Manyara. 

Vijiji hivyo ni miongoni mwa vijiji 10 vinavyoizunguka Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (BWMA) ambavyo awali viliathiriwa na ujangili wa viumbepori ikiwemo ukataji miti kwa ajili ya nishati ya mkaa kwa matumizi ya majumbani.

Biashara ya bidhaa za utamaduni ni matokeo ya historia ndefu ambayo kwa sehemu inatokana na uwepo wa biashara haramu ya mazao ya misitu katika ushoroba wa Kwakuchinja kwa zaidi ya miaka 15. 

Awali baadhi ya wanawake wanaouza bidhaa hizo walikuwa wakijishughulisha na biashara iliyohusisha uharibifu wa bioanuai kama ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa na uuzaji wa nyamapori kinyume na sheria. 

Cesilia Philipo (62), mzaliwa na mkazi wa kijiji cha Vilimavitatu, ni miongoni mwa akina Mama hao walioamua kuachana na biashara haramu ya ukataji wa miti na kufanya biashara rafiki wa mazingira ya kutengeneza na kuuza bidhaa za mikeka. 

Cesilia anasema biashara za kitamaduni anazotengeneza kwa kutumia mikeka kama vile majamvi na vikapu ambayo hupendwa zaidi na watalii wa ndani na nje, ameianza miaka 15 iliyopita baada ya kupitia changamoto mbalimbali wakati akifanya biashara haramu ya uuzaji wa mkaa. 

Kijiji hicho anachokaa Cesilia ni miongoni mwa vijiji 10 vilivyounda Jumuiya ya Uhifadhi ya Burunge ambapo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Vilimavitatu Aboubakar Msuya ambaye anaeleza kuwa nafasi ya kijiji chake ni kulinda na kuhakikisha mazingira salama ya uhifadhi. 

Kipindi cha nyuma, Msuya anakiri kuwa kijiji hicho kiliathiriwa na shughuli za binadamu ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa, lakini baada ya uanzishwaji wa jumuiya hiyo pamoja na utungwaji wa sheria ndogo ya mazingira hali imebadilika. 

Amesema kwa sasa wale waliokuwa wanauza mikaa wameacha na kugeukia biashara nyingine kama vile uuzaji wa bidhaa za utamaduni, kilimo pamoja uvuvi, na pia imewasaidia kwa sababu wamefanikiwa kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa. 

“Hata mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yanakuja kwa wingi kuwajengea uwezo katika biashara zao, tofauti na hapo awali, wasingeweza kupewa elimu hiyo kwa sababu biashara waliyokuwa wanaifanya ilikuwa ni ya siri,” amesema Msuya. 

Sheria ndogo za uhifadhi za kijiji hicho zinatoza faini ya Shilingi 50,000, kunyang’anya mkaa na kuwatoza watu waliokamatwa gharama za ukamataji. 

Anasema licha ya sheria hiyo kusaidia kutatua changamoto ya ujangili wa misitu, lakini bado anaamini katika kutoa elimu kwani inasambaa na kudumu kwa muda mrefu kwa jamii kuliko kusubiri uharibifu utokee ndiyo mtuhumiwa apigwe faini. 

Ukitoa biashara haramu ya misitu “Biashara ya mkaa ilikuwa ngumu sana, huwezi kuifanya kwa uhuru kwa sababu serikali ya kijiji ilikuwa inanifuatilia, baadaye ikaja hii Jumuiya ya Uhifadhi, hapo ndo mambo yakaharibika kabisa,” amesema Cesilia, 

“Hii jumuiya ilifanya mambo yakawa magumu mno kwa upande wa mkaa, tangu imeanza mwaka 2008 kama sikosei mwaka mmoja tu mimi nikasema siwezi kufanya hii biashara kwa sababu ninaweza kufungwa niache watoto wangu wadogo, nikaachana nayo kabisa” ameongeza Cesilia. 

Cesilia ni sehemu ya mamia ya wanawake Tanzania wanaoishi jirani ya hifadhi za wanyamapori na kuingia kwenye biashara haramu kwa sababu ya kusaka vipato ili waweze kujikwamua na umasikini. 

Lakini pia ni miongoni mwa wanawake nchini walioamua kuachana na biashara haramu ya mazao ya misitu na kufanya biashara halali kama ya bidhaa za kiutamaduni. 

Anasema wakati akifanya biashara ya mkaa alikuwa akikamatwa mara kwa mara na kutozwa faini ya fedha pamoja na kunyang’anywa mkaa jambo lililomfanya ashindwe kupiga hatua kimaendeleo. 

“Kitu kikishaitwa biashara haramu achana nacho, unaweza ukauza mzigo ukapata faida kubwa, lakini siku ukikamatwa unalipishwa faini kwa hiyo hela yote uliyokusanya unaitumia kulipa faini, lakini mbaya zaidi hata mzigo ulionayo unachukuliwa, unaanza tena upya,”

 Awaepusha wenzie na balaa 

Kutokana na changamoto hizo Cesilia hakuwa mchoyo wa kuhamasisha wanawake wenzake kuachana na biashara haramu ya mazao ya misitu na hata kuwapa ujuzi wa kutengeneza bidhaa za kiutamaduni. 

Tumaini Jasper (48) ni miongoni mwa wanawake walioamua kuachana na biashara ya mkaa na kufanya biashara ya mikeka kupitia kwa Cesilia. 

Tumaini anasema amefanya biashara ya mkaa kwa miaka nane, licha ya kukumbana na changamoto za mara kwa mara kama vile kupokonywa mkaa na kupigwa faini lakini hakuona biashara mbadala hadi alivyomuona Cesilia amefanikiwa. 

“Siyo kwamba kwa miaka hiyo nane nilikuwa nafurahia biashara yangu, hapana, bali sikujua nifanye nini, lakini baada ya mama Cesilia kufanya na kuanza kutuhamasisha ndiyo nikajua kumbe inawezekana,” amesema Tumaini. 

Kwa sasa Tumaini anaweza kupata oda ya kuuza bidhaa ya kuanzia shilingi 200,000 hadi 800,000 kwa mkupuo. Kutokana na kipato alichonacho kwa sasa Tumaini anaweza kujiunga na kikoba, kusomesha watoto shule binafsi na kumudu mahitaji mbalimbali ya familia. 

Tofauti na biashara haramu, Cesilia anasema biashara ya bidhaa za kiutamaduni anazofanya kwa sasa zimempa faida zaidi ya zile haramu kwa kuwa muda mwingi mamlaka zilikuwa zinamwinda. 

 “Lakini sasa hivi nipo huru sana, tena wateja wangu ni pamoja na wale wale waliokuwa wananikamata,” anasema Cesilia. 

Kwa sasa Cesilia ni mwanachama wa kikundi cha Mdori Group kilichodhaminiwa na asasi ya kiraia ya Chemchem Association inayotekeleza mradi unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. 

Biashara mbadala yamtoa kimaisha
Licha ya kutotaka kutaja kipato chake halisi kwa mwezi lakini Cesilia amekiri kuwa biashara hii imemsaidia kujenga nyumba anayoishi yeye na familia yake, kusomesha watoto pamoja na kuendesha maisha yao ya kila siku. 

“Kupitia biashara hii nimefanikiwa kusomesha watoto, wawili wamemaliza kidato cha nne na wengine wameishia elimu ya msingi, lakini pia nimeweza kujenga nyumba ninayoishi, ninaweza kumudu gharama za maisha za familia yangu,|” Amesema. 

Ufanyaji wa biashara halali kama hizo unasaidia watu wengi Tanzania kuondokana na umaskini. 

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2017/18 za utafiti wa bajeti ya kaya (Household budget survey) umeonyesha kiwango cha umasikini wa chakula na mahitaji muhimu kwa mwezi kwa watu wazima Tanzania Bara kimezidi kupungua mwaka hadi mwaka. 

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kiwango kimeongezeka kutoka Shilingi 33,748 kwa mwaka 2017 mpaka kufikia Shilingi 49,320 mwaka 2018. 

Malighafi bado mtihani Sehemu kubwa ya wanawake wanojishughulisha na biashara mbadala kama kufuma mikeka wanakumbana na uhaba mkubwa wa malighafi kwa kuwa bidhaa hizo pia hutengenezwa na mimea ambayo ni viumbepori.

Cesilia anasema licha ya mafanikio aliyonayo lakini anakumbana na changamoto ya upatikanaji wa malighafi ya kutengeneza mikeka maarufu kwa jina minyaa ambayo inapatikana ndani ya hifadhi ya Jumuiya ya Burunge. 

Burunge WMA imepiga marufuku watu kuingia hifadhini

 Kutokana na kadhia hii, ameiomba mamlaka husika iwatambue wauzaji wa mikeka kama wahifadhi wa maliasili na kuwawekea mazingira mazuri kwa ajili ya kuingia hifadhini kwa ajili ya kukata minyaa.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu endelevu za uhifadhi kwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ili kufanya kuwa endelevu. 

Wadau waongeza nguvu uhifadhi

Afisa Tawala Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kutoka Chem Chem Association, Ernest Elia amesema taasisi hiyo imejikita katika kuwainua wanawake kiuchumi kwa kushirikiana na wabia wao taasisi ya Hand in Hand International iliyoanza mwaka 2023. 

Anasema kupitia washirika hao wanatoa elimu aina mbalimbali ya kujiingizia kipato ikiwemo VIKOBA, ufugaji wa kuku na nyuki kwa wanawake wa vijiji vyote 10 inavyounda Burunge WMA kwa lengo la kupunguza utegemezi wa malighafi kutoka ndani ya hifadhi. 

Anasema kabla ya kutoa elimu hiyo walifanya upembuzi yakinifu kwa kushirkisha mawazo ya akina mama hao ili kujua ni aina gani ya biashara wanaweza kufanya kulingana na mazingira yao. 

“Tangu wameunda vikoba mwaka 2020 tumefanikiwa sana kupunguza utegemezi wa malighafi kutoka msituni kama vile miti kwa ajili ya mkaa, kwa hiyo bado tunaendelea kutoa elimu pamoja na kuwawezesha kiuchumi, naamini ipo siku suala la ujangili wa mazao ya misitu litaisha,” amesema Elia. 

Serikali kuendelea kuwawezesha wanawake 

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Tangwe amesema kupitia vikao vya mara kwa mara vya ujirani mwema na vijiji vilivyozunguka uhifadhi wamefanikiwa kupunguza ujangili wa mazao ya misitu kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na wawekezaji kuwapatia mafunzo na biashara mbadala. 

Amesema serikali imeendelea kuhamasisha jamii hasa wanawake kujiunga vikundi ili kujengewa uwezo wa kuwa na sifa za kukopeshwa fedha kupitia programu ya mfuko wa mikopo kutoka halmshauri.

 “Ingawa kwa sasa zoezi limesitishwa kwa muda kwa ajili ya kuboresha zaidi mikopo hiyo, lakini kundi la kina mama limekuwa likipewa kipaumbele katika mikopo hiyo, mbali na mikopo hiyo hata wadau waliopo hapa Babati wamekuwa wakitoa sapoti kubwa kwa akinamama wetu,” amesema Tangwe. 

Sera ya wanyamapori ya Tanzania ya mwaka 2007 inaitaka serikali na wadau wa uhifadhi kulinda shoroba za wanyamapori, njia za uhamiaji, maeneo ya usalama wa wanyama na kuhakikisha jamii zilizo katika maeneo hayo ya wanyama zinafaidika vilivyo kutokana na uhifadhi wanyamapori.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post