KAIRUKI: DHAMIRA YA SERIKALI NI KUVUTIA WATALII ZAIDI NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki akizungumza na Wadau wa Utalii katika maonyesho ya KARIBU-KILIFAIR 2024 jijini Arusha
 
Egidia Vedasto
 Arusha.

Waziri wa Maliasili na utalii, Angellah Kairuki amesema dhamira ya serikali ni kuendelea kuutangaza utalii wa Tanzania duniani kote ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutalii nchini. 

Kairuki ametoa kauli hiyo wakati akizindua maonesho ya Karibu-Kili Fair 2024 leo Juni 07, 2024 kwenye Viwanja vya Magereza Mjini Arusha.

Amesema serikali pia inatambua mchango wa sekta binafsi katika jitihada za kukuza na kuutangaza utalii wa Tanzania. 

Aidha Kairuki amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuutangaza utalii kupitia Makala ya The Royal Tour na Amaizing Tanzania suala ambalo limeongeza idadi ya watalii wanaofika kutalii nchini Tanzania.

Waziri Kairuki ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa utalii wakiwemo mawakala wa usafiri ili kuhakikisha wanawezeshwa na wanakuwa sehemu ya mabalozi wa utalii watakaokuwa na jukumu la kuutangaza utalii wa Tanzania. 

"Kipekee naipongeza Kampuni ya Kili Fair Promotion Ltd kwa kuandaa maonesho ya Karibu Kili Fair 2024, onesho ambalo limekuwa likiongeza idadi ya watalii wanaofika nchini Tanzania na kuifahamisha dunia kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania"amesema Kairuki. 

Waziri Angellah Kairuki (katikati)akiwa katika gari la kampuni ya HANSPAL pamoja na viongozi wengine akiwemo Mkuu wa mkoa Arusha Paul Makonda (kushoto), Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya KILIFAIR Promotion LTD Dominic Shoo (Kulia).

Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi anatarajia kuzindua mradi wa uwekezaji katika visiwa vidogo 52 vilivyopo Kisiwa cha Bawe 15 Juni mwaka huu. 

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Visiwani Zanzibar Mudrick Ramadhan Soraga wakati akihutubia kwenye uzinduzi wa onyesho hilo huku akiwakaribisha washiriki wa onesho hilo kuhudhuria uzinduzi huo ikiwa ni mpango maalum wa kuvihuisha visiwa vidogo vinavyopatikana kwenye visiwa vya Unguja na Pemba. 

Amesema Mwaka 2021 serikali ya Zanzibar iliruhusu uwekezaji kwenye visiwa vidogo vilivyopo Unguja na Pemba ikiwa ni utekelezaji wa sera ya serikali ya kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya utalii na uchumi wa buluu ili kuongeza pato la Taifa.

"Nakupongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kwa kutambulisha na kumuomba Rais Mwinyi kusaidia katika kuiunganisha Zanzibar na Arusha kiutalii, mpango huo utasaidia katika kuongeza pato la Taifa kupitia sekta hii ya Utalii yenye kuingiza fedha nyingi za kigeni" amesema Soraga.

Pia Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Kili Fair Promotion Ltd Dominic Shoo, ambao ni waandaaji wa onesho la kimataifa la Karibu Kili fair 2024 amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Arusha na Afrika Mashariki kwa ujumla.

"Msimu huu wa 9 zaidi ya makampuni 450 yameshiriki kutoka Tanzania, Ghana,Burundi, Cameroon na Afrika Kusini huku makampuni zaidi ya 700 kutoka nchi zaidi ya 40 wakishiriki"amesema.

"Maonyesho hayo yatakayodumu kwa siku tatu mfululizo yanatoa fursa ya kiuchumi kwenye sekta ya kilimo, Usafiri, utalii pamoja na kubadilishana uzoefu kutokana na wingi wa wageni na wadau wa utalii wanaotarajiwa kuhudhuria maonesho hayo makubwa kwa Afrika Mashariki" amesema Shoo.

Mmoja wa washiriki Kutoka kampuni ya Temple Point Hotel iliyopo eneo la Watamu nchini Kenya Mike Mutiga amepongeza uwepo wa maonyesho haya kwani yanatoa nafasi kubwa kwa wadau wa utalii kubadilishana ujuzi, maarifa na mbinu katika utendaji kazi wao.
Mike Mutiga (kushoto) Meneja Mauzo kutoka Kampuni ya Temple Point Hotel ya nchini Kenya.

"Kwangu hii ni mara ya kwanza kushiriki haya maonyesho lakini nategemea kunufaika pakubwa jinsi nitabadilishana uzoefu na kukutana na watu wengi zaidi" ameeleza Mutiga. 

Naye Cynthia Otoro kutoka Shirika la ndege la Jambojet la nchini Kenya amesema hivi karibuni wanatarajia ndege hiyo kufanya safari zake kutoka Visiwa vya Zanzibar kwenda Mombasa mara nne kwa wiki.
Watendaji wa shirika la ndege la Jambojet kutoka nchini Kenya (kulia) ni Cynthia Otoro.

"Nifuraha yetu kubwa kuunganisha watalii kati ya miji hii miwili mashuhuri, tunaamini uchumi wetu utakua kwa pande zote mbili Kenya na Tanzania" amefafanua Otoro.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post