Wawakilishi wa Tanzania Mkutano wa PAPU waitetea nchi yao

Na Mwandishi Wetu,

 Arusha 

Vikao vya Kamati za Ufundi vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) vimeendelea katika siku ya tatu  jijini Arusha, ambapo Tanzania imewasilisha hoja zake mbalimbali ikiwemo kupendekeza kuwa na Mwakilishi kiongozi katika nafasi ya juu ya uongozi wa Umoja huo.

Hoja hiyo imetolewa na wawakilishi hao ikizingatiwa kuwa mkataba wa nchi mwenyeji inatakiwa kuchangia asilimia 50 ya bajeti ya uendeshaji ya PAPU kila mwanzo wa mwaka wa fedha iwapo nchi wanachama hawajachangia kwa wakati, fedha ambazo baadaye hurejeshwa.

Pendekezo hilo limetolewa leo tarehe 05 Juni, 2024 na wawakilishi wa Tanzania katika Kamati ya Fedha na Utawala kwenye Vikao vya Wataalam wa masuala ya Posta vinavyoshirikisha wajumbe kutoka mataifa 46 wanachama wa  PAPU.

Vikao hivyo vilivyoanza Jumatatu 03 Juni, 2024, vinawajumuisha wajumbe waliowasili Arusha na wanaoshiriki kwa njia ya  mtandao,  vikiwa ni vikao vya utangulizi wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU utakaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 12 Juni, 2024.

Aidha, wajumbe hao katika hoja zao wamesisitiza kuipata nafasi hiyo ili kuhakikisha usimamizi imara wa fedha zinazotolewa ambazo Tanzania imekuwa ikilipa kama nchi mwenyeji na pia kusimamia kikamilifu ili kupata marejesho ya gharama za ujenzi ilizolipa zaidi ya kiwango chao cha umiliki cha asilimia 40 (40%).

Katika mjadala huo pia Tanzania imehoji nchi wanachama ambao hawachangii ada ya uanachama lakini zinanufaika kutoka kwa nchi zinazoonesha  uaminifu wa kulipa ada zao kila mwaka kama Tanzania.

Taarifa ya fedha inaonesha ni nchi 25 tu kati ya nchi 46 wanachama wa PAPU ndizo zinazoonesha uaminifu wa kulipa michango hiyo ya lazima hali inayodumaza shughuli mbalimbali za Umoja huo.

Kwa upande wa Kamati ya Mkakati (Strategy), wajumbe walionesha mchango mkubwa wa Tanzania katika ujenzi wa jengo la PAPU lililo Jijini, Arusha ambapo mwaka huu Mkutano wa 42 wa Baraza la Umoja wa Posta Afrika unafanyika. 

Kuhusu utatuzi wa majanga, nchi wanachama zimetakiwa kutoa taarifa ndani ya saa 48 baada ya majanga kutokea ili kupata usaidizi wa haraka huku pia Posta yenyewe ikishiriki kutoa misaada hiyo pale inapoweza.

Kamati hii imefikia maazimio ya kuunda Kikosi kazi katika Kamati ya Mkakati kitakachoshughulikia Upanuzi na Ushirikishaji watoa huduma katika Sekta ya Posta ambapo Tanzania imejitolea kushiriki pamoja na nchi za Botswana, Burkina Faso, Cameroon, DRC, Ivory Coast, Kenya, Misri, Namibia, Niger, na Uganda.

Wajumbe hao pia wamejadili masuala ya mapato na matumizi ya umoja, miradi, ajira na stahiki za watumishi wazawa, michango ya ada za uanachama na Mpango Mkakati wa miaka minne wa sekta ya Posta barani Afrika ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post