Maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza kufuatilia Ligi ya Krismas CUP inayoendelea katika Uwanja wa Mhangu, Kata ya Salawe, Wilaya ya Shinyanga vijijini.
Mashindano haya yameandaliwa na Makamba Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka, kwa lengo la kuibua vipaji vya michezo mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani.
Ligi hiyo inajumuisha jumla ya timu 16, ambapo leo imechezwa mechi ya saba kati ya Mwagiligili FC na Mahando FC, timu zote kutoka Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.
Katika mchuano huo, Mahando FC wameibuka washindi kwa ushindi wa mabao 3-2 ambapo wafungaji wa Mahando FC ni Ramadhan Vita aliyepachika mabao mawili na Hamis Hamis aliyekamilisha ushindi, huku Mwagiligili FC wakijibu kupitia mabao ya Thomas Mula na Miyco Michal.
Awali, kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kwa wasichana wa Sekondari ya Mhangu dhidi ya Salawe, ambapo dakika 90 za kawaida zilimalizika kwa sare ya 1-1. Hatimaye, Mhangu Girls waliibuka washindi kwa mikwaju ya penati 3-2 na kutwaa zawadi yao.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, amesema mashindano hayo yanaendelea vizuri huku wachezaji wakionesha nidhamu ya hali ya juu ambapo ameendelea kuhimiza wananchi, viongozi, na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kufuatilia mechi hizo.
Mwalimu Kijida amebainisha kuwa kesho kutakuwa na mechi ya nane, kati ya Modern FC na Mwasenge FC, ambayo itahitimisha hatua ya mtoano kabla ya kuingia kwenye robo fainali.
Baadhi ya viongozi ambao wamehudhuria mashindano hayo wameendelea kumpongeza Makamba Lameck kwa kuandaa ligi hiyo inayowavutia wananchi kwa kiingilio cha bure, tofauti na mashindano mengine.
Mashindano haya yanatarajiwa kufikia kilele chake Disemba 17, 2024.
Endelea kufuatilia ligi hii kupitia mitandao yetu ya kijamii kwa jina la MISALABA MEDIA.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, akizungumza.
Makamba Lameck mdau wa Michezo ndiye mwandaaji na mdhamini wa ligi ya Krismas CUP kupitia kampuni yake ya MCL, inayojihusisha na biashara ya nafaka.