Mtaalam wa mionzi Alex Mpugi akitoa maelezo jinsi mashine ya mionzi inavyofanya kazi
Mashine ya kisasa ya kutambua(kupanga) sehemu inayotakiwa kupatiwa mionzi iliyoko kwenye hospitali ya kanda ya rufaa Bugando
Maofisa habari wakielekezwa kifaa cha mionzi cha shingo ya kizazi
Mkurugenzi wa upasuaji wa BMC Dkt.
Fabian Massaga akifafanua jambo wakati maofisa habari wa wizara ya afya
na taasisi zake walivyotembelea idara hiyo ambapo hivi sasa wamepunguza
idadi ya wagonjwa kusubiri upasuaji kutoka miezi mitatu hadi ndani ya
wiki moja
Picha ya pamoja ya maofisa habari
kutoka wizara ya afya na taasisi zake mara baada ya kutembelea idara ya
upasuaji na kujionea maboresho makubwa ikiwemo upanuzi wa vyumba vya
upasuaji kutoka sita hadi kumi na tatu pamoja na vifaa na vifaa tiba vya
kisasa
…………………
Na.Catherine Sungura-Mwanza
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya
Bugando (BMC) imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni mbili kwa
wananchi wa kanda ya ziwa kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam kupata
matibabu ya saratani kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu
wa Hospitali hiyo Prof. Abel Makubi wakati akiongea na Maofisa habari wa
Wizara ya Afya na Taasisi zake waliokuwepo jijini Mwanza kwa ajili ya
kujionea mafanikio ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Prof. Makubi alisema kuwa kuanza
kwa tiba ya saratani katika Hospitali ya Kanda Bugando imesaidia kuokoa
kiwango cha fedha hizo kutoka kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambapo awali
iliwalazimu kusafiri hadi Jijini Dar es Salaam kupata huduma hizo
kwenye Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.
“Tunaishukuru Wizara ya Afya
ambayo ilitupatia kiasi cha Shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kujenga
jengo la saratani. Kama hospitali tumeweza kununua mashine nne za mionzi
na dawa kwa kushirikiana na wafadhili wengine”.
Aidha, alisema, hivi sasa asilimia
90 ya wagonjwa hawapelekwi wanapata huduma hapa hivyo kuwaondolea adha
ya kusafiri na kupata huduma mbali wananchi wa kanda ya ziwa ambapo
awali zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wa saratani wa Ocean Road
walikuwa wakitoka kanda hiyo.
Naye Mtaalam wa Tiba Mionzi wa
Idara ya Saratani wa BMC, Alex Mpugi alisema kabla ya mashine hizo
walikua wakitoa huduma za saratani kwa kutumia kemikali.
“Naomba nitoe wito kwa wananchi
hususan wanawake kujitokeza kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya
uzazi na matiti kila siku ya Jumanne na Alhamis”.Alisisitiza Mpungi.
Kwa upande wa Upasuaji Mkurugenzi
wa Upasuaji Dkt.Fabian Massaga alisema kuwa,Hospitali imefanikiwa
kufanya ukarabati na upanuzi wa vyumba vya upasuaji kutoka vyumba sita
hadi kumi na tatu ambapo vyumba viwili hutumika kwa upasuaji wa dharura
na kimoja kwa ajili ya upasuaji kwa akina mama wajawazito.
Aliongeza kuwa kwa upande wa
upasuaji wameweza kuongeza idadi ya wagonjwa kutoka ishirini na tano
hadi hamsini na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wengi waliokuwa
wanasubiri upasuaji kwa miezi mitatu lakini hivi sasa wanafanyiwa
upasuaji ndani ya wiki moja.
Hata hivyo Dkt. Massaga alisema
upanuzi huo umeendana na ununuzi wa vifaa vipya na vya kisasa ikiwemo
vitanda vya kufanyia upasuaji, taa maalumu za vyumba vya upasuaji na
mashine za kisasa kabisa za kutolea dawa ya usingizi. Vifaa hivi
vimeagizwa moja kwa moja viwandani kwa takribani Shilingi bilioni 1.4
badala ya Shilingi bilioni 3 kama wangenunua kwa wauzaji hapa nchini.