NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
JESHI la polisi
mkoani Pwani, limekamata madumu 859 ya mafuta ya kula yanayodaiwa
kutolipiwa ushuru ,yenye thamani takriban milioni 50 ,huko Chemchem kata
ya Magomeni ,Bagamoyo.
Akithibitisha kuhusu
tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani hapo,Wankyo Nyigesa alisema ,madumu
hayo yalikuwa yakisafirishwa na Christopher Emmanuel (32).
Alieleza kuwa,
Christopher aliyasafirisha madumu hayo kupitia gari yake namba T.621 BCG
aina ya fuso baada ya kukwepa kulipa ushuru kwenye moja ya bandari bubu
Bagamoyo.
“Tunachunguza risiti
zake za malipo kwani pia zina TIN namba tofauti,tunamshikilia mtu huyu
pamoja na aliyeshirikiana nae kutoa Hassan Saidi mpemba huyu mkazi wa
Bagamoyo.”
Wankyo alisema, huo
ni usafirishaji haramu na kulitia hasara Taifa kwa kukwepa kulipa ushuru
ama kodi,hivyo aliwaasa wananchi kuacha biashara za magendo.
Kamanda huyo alifafanua, wafanyabiashara wanapaswa kulipa ushuru kwa maendeleo ya Taifa na sio kutaka faida kwa njia za mkato.
Alibainisha
hawatawaachia nafasi wakwepa ushuru na kudhibiti mianya ya kukwepa
ushuru kwenye bandari zote bubu kwakuwa zinafahamika.