Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania,
Mohammed Othman Chande akitoa Lecture kwa wanasheria wachanga kuhusu
majukumu yao kwa jamii na taaluma hiyo wakati wa sherehe ya majadiliano
baina ya wanafunzi hao iliyofanyika katika chuo cha sheria jijini Dar es
Salaam.
Balozi Juma Mwapachu
akizungumza na wanasheria wachanga wakati wa sherehe ya majadiliano
baina ya wanafunzi wa sheria, iliyofanyika mijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi
wa haki za binadamu (TDHRC), Onesma Olengurumwa akizungumza wakati wa
sherehe ya majadiliano baina ya wanafunzi hao iliyofanyika katika chuo
cha sheria jijini Dar.
*********************************
NA EMMANUEL MBATILO
JAJI Mstaafu wa Mahakama Kuu
Tanzania, Mohamed Chande Othman amewataka mawakili watarajiwa kwenda
kufanya kazi vijijini kama maofisa wa mahakama wakasaidie katika utoaji
haki kwani asilimia 70 za kesi nchini zipo Mahakama za Mwanzo lakini
wananchi wanajiwakilisha wenyewe.
Jaji Chande ameyasema hayo wakati
akitoa mhadhara (Lecture) wa Jukumu la wanasheria chipukizi kwa umma na
mwelekeo wa sekta ya sheria Tanzania kwa wanasheria wachanga jijini Dar
es Salaam walipokutana pamoja kujadiliana mambo mbali mbali ikiwemo
kuhamasisha wanasheria wachanga ambao bado hawajasajiliwa na wale
waliosajiliwa kufanya kazi kwa weledi.
Amewaambia kuwa wakiwa kama
wanasheria vijana wanapaswa kuhakikisha wanafikia wananchi waliopo
vijijini ili kuwasaidia katika masuala yao ya kisheria na kusaidia
mahakama katika utoaji haki kwa haraka zaidi kwani mawakili wengi
wamekuwa wakiishia kufanya kazi mijini kuliko vijijini.
Pia amewataka kuhakikisha kuwa
wanafanya kazi kwa kuafuata maadili yao kwa kuwa wakweli na kuepuka
vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanalinda utawala wa sheria na haki za
msingi, uhuru na wajibu.
“Katika Mkoa wa Lindi, kuna wakili
mmoja huku mawakili nane wakiwa katika Mkoa wa Katavi, 20 mkoani
Ruvuma, 29 Kigoma na 38 wapo mkoani Mara.
Aidha Jaji Chande amesema kuna
baadhi ya mikoa takribani saba ya Tanzania Bara haina Mahakama Kuu kama
vile, Lindi, Katavi, Morogoro, Simiyu, Manyara, Pwani, Singida and
Songwe huku Wilaya 28 zikiwa hazina Mahakama za Wilaya kama vile Mkinga.
“Kutokuwepo kwa mahakama ni
kikwazo kikubwa katika utoaji wa haki na masuala ya sheria hususani kwa
mawakili wachanga. Hivyo, tutaendelea kuishauri serikali kuharakisha
ujenzi wa miundombinu ya mahakama ili watu waweze kupata haki zao
natambua kuna mchakato wa mahakama wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na
mahakama,” amesema Jaji Chande.
Amefafanua kuwa katika ripoti ya
dunia ya mwaka 2019 kuhusu utoaji haki inaonesha watu milioni 230
wanaoishi katika mazingira mbalimbali wanakosa haki huku watu bilioni
1.5 wanashindwa kutatua matatizo yanayowakabili yanayohusu haki na watu
bilioni 4.5 wametengwa na fursa zitolewazo na sheria na inaonesha
kutokuwepo kwa usawa au ufikishaji sawa wa haki kwa wote na ukosefu
mkubwa wa uwakilishi wa kisheria.
Jaji Chande amesema katika miaka
mitano iliyopita zaidi ya asilimia 50 ya mawakili wamepokelewa nchini
kufanya kazi hivyo, anaamini wataendelea kubadilisha muundo na taasisi
ya sheria.
Kwa upande wake Balozi Juma
Mwapachu amesema serikali imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha
miundombinu ya mahakama lakini bado watu wengi wana uhitaji wa kusaidiwa
katika masuala ya utoaji haki.
“Wanasheria wachanga wanatakiwa
kujua wanaisaidiaje jamii katika masuala ya sheria pamoja na kupigania
haki za binadamu, uhuru wa kuongea na katiba” amesema.
Naye, Mratibu wa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za binadamu (TDHRC), Onesmo Olengurumwa amesema ni
wakati wa mawakili kuhakikisha wanakwenda vijijini kuwasaidia wananchi
waliowengi ambao hawajui masuala ya sheria.
Amesema, wanasheria wanapaswa kuwa
na wito na uelewa mkubwa katika kuendesha kesi zenye maslahi kwa umma
na zile za ki mkakati zaidi.
Olengurumwa ameongeza kuwa, kwa
sasa kuna changamoto kubwa kwa mawakili kurundikana mijini, kwani nchini
kuna mawakili wapatao 8000 lakini nusu ya hao wako mijini hivyo
wanapaswa kujua wameitwa katika kazi hivyo kusaidia watu wote.