Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe, Ally
Hapi amewataka vijana nchini kutumia muda wao kufanya kazi zenye tija
kiuchumi badala ya kukesha kwenye mitandao ya kijamii wakituma na
kubishana mambo yasiyo na tija kwao na kwa taifa.
Mhe, Hapi ameyasema hayo leo wakati akifungua kongamano la fursa za kiuchumi kwa vijana zaidi ya 500 wa Wilaya ya Kilolo.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya
tano chini ya Mhe, Rais Dkt John Magufuli, imejipanga kuwawezesha
wananchi kiuchumi na kwa upande wa vijana ,wanawake na walemavu kuna
fedha za mikopo kupitia Halmashauri inayotolewa ambako kwa Mkoa wa
Iringa takribani bilioni 1.2 imetolewa kwa mwaka 2018/2019.
RC.Hapi
amewataka vijana kuchangamkia fursa za mikopo hiyo badala ya kupoteza
muda kwa mambo ya hovyo mitandaoni na vijiweni.
”Taifa letu linawategemea vijana,
nyinyi ndio nguzo ya uchumi wa taifa. Hamna budi kutumia muda wenu
vizuri kwa mambo yenye tija kwenu kiuchumi…” Alisema RC.Hapi.
Aidha, RC.Hapi amezitaka
halmashauri za Iringa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wanaopewa mikopo
ili wawe na uwezo wa kufanya biashara kwa ufanisi na kurejesha mikopo
hiyo.
Hapi amezitaja fursa za kiuchumi
kwa vijana kuwa zipo nyingi zikiwemo za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa
ambapo soko kubwa la maziwa lipo kwenye kiwanda cha ASAS Iringa ambacho
kina uhitaji mkubwa wa maziwa huku maziwa wanayopata yakiwa
hayatoshelezi mahitaji ya kiwanda.
Hata hivyo RC Hapi alisema mkoa wa
Iringa unajiandaa kwa kulitumia shamba la mitamba la Sao Hill Mufindi
kwa kuzalisha na kukopesha Ng’ombe kwa makundi mbalimbali ili kuwezesha
kukuza sekta ya maziwa kama chanzo cha kipato.