RC MAKONDA ATAJA ANAKOTOA PESA ZA KUTOA MISAADA KWA WATU


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema kuwa pesa ambazo huwa anaonekana akizigawa ni pesa ambazo anazipata kwa wadau na marafiki zake wa karibu ambao wako tayari kumuunga mkono katika masuala ya maendeleo.

Makonda ameyabainisha hayo leo Septemba 18, alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, walipokuwa wametembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kujionea utendaji kazi wa Taasisi hiyo na kupokea taarifa ya watoto ambao wamekwishapatiwa matibabu, kutokana na utaratibu wake aliouweka wa kusaidia watoto 10 kila mwezi.

“Mheshimiwa waziri (Ummy) kuna watu wanasema huyu Makonda anatoa wapi  hela, kwa mfano zile fedha milioni 10 za Juma Kaseja zimepigiwa kelele kwelikweli..ooh kapiga penati kapewa milioni 10.


“Jamani nchi hii ni tajiri na watu wa nchi hii ni tajiri pia, inahitajika tu mtu mwaminifu mwadilifu anayeomba pesa kwa matumizi sahihi na watu wao wanatoa pesa. Balozi huyu wa Falme za Kiarabu yupo ana marafiki wengi lakini huwa namuona wengine wanakunywa naye kahawa basi….” amesema

Aidha Makonda yupo katika mchakato wa kuunda kamati maalumu ya kufunga mwaka, yenye mlengo wa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 1, kutoka katika makampuni mbalimbali, fedha zitakazosaidia kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo ya moyo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post