ARSENAL YAMTEUA ARTETA KUWA KOCHA

Arsenal imemteua kiungo wake wa zamani Mikel Arteta kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo.

Kocha huyo mwenye miaka 37 ameshinda kombe la FA mara mbili akiwa na kikosi cha Gunners katika misimu mitano aliyokipiga na vigogo hao wa London.

Anachukua nafasi ya Mhispania mwenzake, Unai Emery ambaye alitimuliwa mwezi Novemba kutokana na matokeo mabovu.

Arteta anatokea Manchester City ambapo kwa miaka mitatu alikuwa kocha msaidizi wa Pep Guardiola.

"Tunahitaji kuwa tunagombea mataji makubwa," amesema Arteta.

"Suala hilo limebainishwa wazi katika mazugumzo yangu na (wamiliki wa Arsenal) Stan na Josh Kroenke na watu wengine waandamizi ndani ya klabu."

Arteta hata hivyo atachukua usukani rasmi siku ya Jumapili, akimuachia Freddie Ljungberg kuendelea kukaimu nafasi ya ukocha kwenye mchezo dhidi ya Everton kesho Jumamosi.

Arsenal kwa sasa wapo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi ya Primia wakiwa na alama 22.

"Wote tunajua kuwa kuna kibarua kigumu hapa cha kufanyika ili kuleta mapinduzi, na nina imani kuwa tutafanikiwa. Najua pia kuwa mabadilikoo hayatatokea kwa siku moja, lakini kikosi cha sasa kina vipaji vingi na kuna bomba la wachezaji wadogo wanaokuja kutoka kwenye akademi."

Arsenal ilizidi kudidimia baada ya kukubali kipigo cha 3-0 kutoka kwa Man City siku ya Jumapili.

Arsenal sasa imecheza mechi tano bila ushindi katika dimba la nyumbani la Emirates, ikiwa ni ukame mkali zaidi wa ushindi wa nyumbani toka mwaka 1995.

Chanzo- BBC

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post