Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowea,amehudhuria maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru katika Uwanja wa CCM Kirumba,jijini Mwanza.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni hakuvaa sare maalum za chama wala kombati
ambazo zinatumiwa kama vazi maalum chama chao lakini amepigilia suti
nyeusi, shati jeupe na tai. Viongozi wengine wa CHADEMA,CUF na vyama
vingine vya siasa wamehudhuria maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru na miaka
57 ya Jamhuri.
Akizungumza
baada ya Rais Magufuli kuwakaribisha viongozi wa vyama vya siasa
waliokuwa wamekaa jukwaa kuu kusalimia wananchi,Mhe. Mbowe ametoa kauli
zifuatazo:
"Nimekuja kuhudhuria maadhimisho
ya miaka 58 ya Uhuru kama Uthibitisho wa Ulazima wa uwepo wa
maridhiano,uwepo upendo,uwepo mshikamano katika taifa letu.
Nawapongeza sana Watanzania kwa siku ya leo na namuomba Mwenyezi
Mungu siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa la watu
wanaopendana,tuvumiliane,tukosoane turuhusu demokrasia tujenge taifa
lenye upendo na mshikamano
Na Mhe. Rais kwa nafasi ya pekee tuna nafasi ya kuweka historia ya
maridhiano katika taifa kwani kuna wengine wanalalamika,wengine
wanaumia,Mhe. Rais tumia nafasi ukaliweke taifa katika hali ya
utengamano" - Mbowe
Akitumia salaam ya chama chake cha
“Haki” Mwenyekiti wa CUF ,Profesa Lipumba amesema pamoja na hatua kubwa
ya maendeleo inayopigwa, ni jukumu na wajibu wa Rais Magufuli na
Serikali kuendeleza misingi ya demokrasia nchini.
Viongozi wengine waliotoa salaam na
kusisitiza mshikamano, umoja na ulinzi wa amani ya Taifa ni mwenyekiti
wa UDP, John Cheyo na mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa, John
Shibuda.
Taarifa ya kushiriki kwenye maadhimisho kwa Mwenyekiti wa CHADEMA
ilitolewa juzi na Kamati Kuu ya chama hicho kwa kumuagiza Mwenyekiti
wake kwenda kukiwakilisha chama hicho kwenye Sherehe hizo za Uhuru.
Hii ni mara ya kwanza kwa CHADEMA kushiriki kwenye maadhimisho ya Uhuru tangu mwaka 2015.