Audrey alikosa fahamu kwa saa sita baada ya mapigo yake ya moyo kusimama
Mwanamke wa Uingereza ambaye alipata mshtuko wa moyo baada ya mapigo
yake ya moyo kuacha kufanya kazi kwa saa sita amefufuka tena katika kile
ambacho madaktari wamesema ni jambo ambalo halijawahi kutokea hapo
kabla.
Audrey Schoeman alipata mshtuko wa moyo alipopigwa na dhoruba ya theluji
wakati anapanda mlima Pyrenees akiwa na mumewe mnamo mwezi Novemba.
Madaktari wanasema huo ndiyo muda mrefu zaidi kwa mtu kuwahi kupata mshtuko wa moyo nchini Uhispania.
Audrey, ambaye kwa sasa anakaribia kurejea katika hali yake ya kawaida,
amesema anatarajia kupanda tena mlima huo msimu wa masika.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 34 anayeishi Barcelona, alianza
kupata matatizo ya kuzungumza hali ya hewa ilipobadilika alipokuwa
akipanda mlima na baadaye akapoteza fahamu.
Hali yake ilizorota zaidi wakati akisubiri kupata huduma za dharura na mume wake Rohan akaamini kwamba mkewe anakufa.
Akizungumza na vyombo vya habari Alhamisi iliyopita, Mumewe Rohan
alikiambia kituo cha televisheni cha TV3: "Nilikuwa najaribu kumgusa,
mapigo yake ya moyo hayakuwa yanapiga kabisa... Sikuweza kuhisi
akipumua."Mume wa Audrey Schoeman, Rohan, ambaye alidhani mkewe amekufa
Timu ya uokoaji ilipofika saa mbili baadaye, joto la mwili la Audrey lilikuwa limeshuka hadi nyuzijoto 18.
Alipowasili katika hospitali ya Vall d'Hebron huko Barcelona, hakuwa na dalili zozote za kurejesha uhai.
Hata hivyo kiwango cha chini cha joto ambacho kilisababisha Audrey
augue, pia kilimsaidia kunusuru maisha yake, amesema daktari wake Eduard
Argudo.
"Alionekana kana kwamba amekufa,"amesema hivyo katika taarifa aliyotoa.
"Lakini tulichokifahamu hasa katika mshtuko wa moyo, tulijua kwamba kulikuwa na uwezekano wa Audrey kufufuka."
Joto la mwili lililinda mwili na ubongo wake usizorote zaidi wakati
akiwa amepoteza fahamu, daktari Argudo amesema, licha ya kwamba alikuwa
anaelekea kufa.
Aliongeza: "Kama angekuwa katika mshtuka wa moyo kwa kipindi hicho kirefu, joto la mwili wake likiwa kawaida, angekuwa amekufa."
Wakiwa katika hali ya kukimbizana na muda, madaktari wa Audrey
waligeukia mashine maalum inayoweza kuondoa damu na badala yake
wakamuingiza hewa ya oksijeni.
Joto la mwili wake lililofikia nyuzijoto 30, walitumia kifaa cha kufanya
moyo uanze kupiga tena, saa sita baada ya kupata huduma ya kwanza.Audrey na Rohan Schoeman na walioshughulika kumpa huduma ya kwanza
Audrey alitolewa hospitali siku 12 baadaye, akiwa tu na matatizo ya
hisia kwa sababu ya kiwango cha joto alichokuwa nacho wakati amepoteza
fahamu.
"Tulikuwa na wasiwasi kuhusu madhara atakayopata katika mfumo wake wa neva," amesema daktari Argudo.
"Hasa ukizingatia kwamba hakuna mtu ambaye moyo wake ulisita kupiga kwa muda kama huo kisha ukuanza tena kufanya kazi."
Akizungumza baada ya kurejea katika hali yake ya kawaida, Audrey anasema hafahamu chochote kuhusu kilichotokea.
"Kwa siku ya kwanza na pili, sikujua kile kinachoendelea, eti nipo katika chumba cha wagonjwa mahututi," amesema.
"Lakini tangu wakati huo, nimekuwa nikijitahidi kusoma zaidi hasa kuhusu
joto la mwili na kwa kweli na hisi furaha sana kuona nilinusurika
kifo."
Audrey anasema anahisi yeye ni mwenye bahati na pia amewashukuru wafanyakazi wa hospitali hiyo.
"Ni kama miujiza na pia madaktari walichangia pakubwa, Audrey amesema.
Ameongeza kwamba kuna uwezekano mkubwa hatarejea tena kupanda mlima katika kipindi hiki.
"Kwa muda huu haitowezekana lakini nina imani kwamba msimu wa masika
nitaweza kuupanda tena. Sitaki tukio hili liwe sababu ya kuachana na
kile ambacho nimekuwa nikikipenda," amesema.
CHANZO - BBC