Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Mandeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema
amekuwa akishangazwa na watu wanaohoji kwanini chama hicho kimekuwa
kikifanyia mikutano yake katika kumbi zenye bei ghali na kusema kuwa
chama hicho hakihubiri umasikini na kwamba wataendelea kuwa juu.
Mbowe ameyabainisha hayo leo
Disemba 17, 2019, wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho,
unaoendelea katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam na kwamba
wao hawataukiri umasikini bali wataendelea kuhubiri utajiri kwakuwa
wanachama wake wengi wamepitia maumivu mengi sana.
"Ukumbi wa Mlimani City
haututoshi tungetamani tungekuwa na ukumbi mzuri zaidi kuliko huu,
lakini hakuna tutabanana humu humu, tuna wivu na chama chetu, tuna wivu
kwa sababu kuna watu wana maumivu makubwa, kunawatu wamefungwa, wamepata
ulemavu sababu ya chama hichi, kuna Ndoa nyingi zimevunjika shauri ya
chama chetu, yote tumeyavumilia sababu tuna ndoto kubwa" amesema Mbowe.
Mkutano huo wa Baraza Kuu la
chama hicho, utajadili na kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na
kuandaa ajenda za Mkutano Mkuu utakaoanza kesho Disemba 18, 2019.