Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro
Serikali
nimewema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/20 kwa kushirikiana
na sekta binafsi, imejipanga kuzalisha jumla ya tani 53,608.2 za mbegu
mbalimbali.
Wazalishaji
hao ni pamoja na Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA), Vituo vya Utafiti,
Magereza na Sekta binafsi. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea na ujenzi wa Mradi wa Kuongeza
Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka.
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 2 Novemba
2019 wakati akifunga mradi wa ubia kwa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji
endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la Sahara wilaya ya Mvomero
mkoani Morogoro.
Amesema
kuwa Sanjali na jitihada hizo, Wizara ya Kilimo imeanzisha kitengo cha
masoko ya mazao ya kilimo ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na
nje ya nchi kwa mazao mbali mbali yanayozalishwa hapa nchini ili mbegu
zitakazozalishwa na kuwa na mafanikio makubwa katika kilimo uweze
kuimarisha kipato cha wananchi.
Takwimu
zinaonesha kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo
umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa
wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya matrekta na asilimia 24
ya wanyama kazi mwaka 2013.
Amesema
kuwa Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua
na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa
mwaka 2013. Aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF)
Wizara imeendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo.
Mhe
Hasunga amesema kuwa pamoja na hayo, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo
ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika kwa kusimamia na
kuhamasisha maendeleo yake hapa nchini ili wakulima waweze kunufaika na
matunda ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika usimamizi madhubuti wa sekta ya
ushirika.
Ameongeza
kuwa Wizara ya Kilimo imeendelea kuratibu utekelezaji wa mikakati ya
maendeleo ya kilimo hapa nchini kwa kuimarisha huduma za utafiti,
upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa
visumbufu vya mazao, huduma za ugani, uongezaji wa thamani na
upatikanaji wa masoko.
Waziri
Hasunga amesema kuwa Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za
kuhakikisha inaongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini.
Jitihada hizo ni pamoja na Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji kukamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa
Umwagiliaji ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa
kuzingatia Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya Rasilimali za Maji.
Aidha,
Wizara ya Kilimo imeendelea kuanisha maeneo ya kipaumbele ya kuongeza
tija kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa
visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya
kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na
kuzalisha teknolojia kwa mazao mbali mbali ukiwemo mpunga.
Amesema,
Wizara imeanza na itaendelea kuipitia Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka
2013 na sheria mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo ambayo yatapaswa
kuhuishwa ili kwenda na hali halisi ya sasa na mwelekeo wa Serikali wa
kubadili kilimo chetu kuwa kilimo cha kibiashara.
Ameongeza
kuwa Mtazamo wa Wizara ni kuwa na Sheria moja itakayosimamia
rasilimaliwatu, matumizi bora ya pembejeo, ardhi ya kilimo na maeneo
mengine muhimu.
Aidha,
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali
inatambua na kulipongeza Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa
Mataifa-FAO, Serikali ya Venezuela, Halmashauri za Wilaya za Kilosa,
Mvomero na Kilombero kwa utekelezaji wa mradi wa ubia wa maendeleo ya
mifumo ya uzalishaji endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la
Sahara.
Kwa
upande wake Muwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa
Mataifa FAO nchini Tanzania Ndg Fred Kafeero ameipongeza serikali ya
Tanzania kwa kuimarisha ushirikiano na Taasisi za kimataifa katika
kuimarisha sekta ya kilimo.
Ameongeza
kuwa mradi huo kwa upande wa Tanzania ulilenga kujenga mifumo yenye
tija na endelevu katika Afrika ili kuboresha uhakika wa chakula na
kuwezesha maendeleo endelevu kupitia mnyororo wa tahamani wa zao la
mpunga miongoni mwa wakulima watoto hususani vijana.
Aidha
amesema kuwa mradi huo ulilenga kukabiliana na changamoto
zinazosababisha uzalishaji mdogo wa mpunga hapa nchini kwa kutambulisha
na kusambaza teknolojia ya kilimo shadidi cha mpunga kwa kutumia njia
kadhia ambazo FAO imetumia katika nchi nyingine.
Mkutano
huo umehudhuriwa pia na Balozi wa Venezuela kwa Kenya na Tanzania Mhe
Jesus Manzanilla Puppo, Naibu waziri wa kilimo na Ardhi wa serikali ya
Venezuela Mhe Jose Gregorio Aguilers Contreras, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Mhe Loata Erasto Olesanare.