Mgeni
Rasmi Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi ( kwa niaba ya Waziri
wa Fedha, Dk Philip Mpango) akimkabidhi mmoja wa Wahitimu Shahada yake.
Na Abby Nkungu, Singida
SERIKALI
imeitaka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kuboresha zaidi mitaala yake
ili iweze kuzalisha wataalamu mahiri wenye ujuzi na weledi kwa ajili ya
kujibu changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Sera ya uchumi wa
Viwanda hivyo kuwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati
kabla ya mwaka 2025.
Rai hiyo imetolewa Desemba 6,2019 na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango mjini
Singida wakati wa Mahafali ya 17 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)
kwa Wahitimu 1,688 wa kozi za Cheti cha Awali, Astashahada, Stashahada
na Shahada kutoka Kampasi za Mwanza, Kigoma na Singida.
Katika
hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema
Nchimbi, Waziri Mpango alisema fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi,
Usimamizi wa biashara na Uongozi wa raslimali watu ambako Kampasi za
Kigoma, Mwanza na Singida zimejikita, ni muhimu katika kuendesha uchumi
wa Taifa; hususan katika kusimamia mapato na matumizi ya fedha za
umma.
Alisisitiza
kuwa Sera ya nchi kwa sasa ni Uchumi wa Viwanda, hivyo umahiri wa
Wataalamu wanaozalishwa na Taasisi hiyo lazima uonekane dhahiri ili
kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda.
"Ili
kukabiliana na changamoto za Usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha
za umma, mahitaji ya soko, ushindani na utandawazi mnapaswa kuboresha
mitaala yenu kukidhi viwango vya Kimataifa katika umahiri badala ya
maarifa tu ili kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa Sera ya
viwanda. Tunahitaji wataalamu wenye weledi, maarifa na umahiri wa kutatua changamoto na si kuongeza changamoto", alifafanua.
Aidha, aliwasihi wahitimu hao kuweka
mbele suala la uaminifu na uadilifu kwa kuwa hiyo ndiyo silaha na dira
sahihi ya maisha yao ya kila siku. “Uhasibu ni taaluma iliyotukuka;
hivyo ni vyema ninyi mliosomea mkazingatia kwa kiwango cha juu miiko,
kanuni na taratibu zinazotawala fani hiyo”.
Alieleza
kuwa kashfa mbalimbali zinazosikika nchini na kwingineko duniani ni
matokeo ya watu kukosa uaminifu na uadilifu. “Mtakapotoka hapa baada
ya kuhitimu masomo yenu, mtakutana na changamoto mbalimbali, ila
mkumbuke ni uadilifu na uaminfu pekee ndio utakaowaongoza katika maisha
yenu yote” ,aliwaasa.
Dk Mpango aliwataka wahitimu hao kutumia
vyema elimu waliyoipata katika kubuni, kuanzisha na kusimamia shughuli
mbali mbali za kibiashara zitakazowasaidia wao na jamii yote ya
Watanzania katika kujiletea maendeleo.
“Hatua mliyofikia iwe chachu ya
kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira
na kujiajiri. Msipojiimarisha, mtajikuta kazi zenu zinachukuliwa na watu
wa nje" alisema na kutoa angalizo;
"Soko letu la ajira rasmi ni dogo na kwa
kweli halikidhi mahitaji ya wahitimu wote nchini. Ili kukabiliana na
changamoto ya soko la ajira, ni vyema mkaelekeza mawazo yenu kwenye
kujiajiri badala ya kuajiriwa".
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa TIA, Bi Luciana Hembe alitaja baadhi ya changamoto
zinazoikabili Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na gharama kubwa za pango
katika Kampasi za Kigoma na Mwanza kutokana na kukosa majengo yao
wenyewe na uhaba wa miundombinu ya majengo Kampasi ya Singida kutokana
na ongezeko kubwa la wanafunzi.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Saidi Chiguma aliwataka wahitimu
hao kuzingatia uadilifu, nidhamu na uzalendo wakati wote ili
kujipambanua na wahitimu wa vyuo vingine.