Na.Farida Saidy,Morogoro
Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) limewataka wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali za
kibinadamu jirani na miundombinu ya umeme kuacha mara moja ili
kujiepusha na madhara yatakayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha
kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na fullshangwe blog,
Kaimu Meneja Mahusiano TANESCO, Leila Muhaji amesema wale wote
wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kuegesha
magari,kulima,kujenga makazi ya kuishi, na kufanya biashara katika
miundombinu ya umeme wanatakiwa kuacha.
Amewatahadharisha wananchi kutoshika au kukanyaga nyaya za umeme zilizoanguka hususan katika kipindi hiki cha mvua.
“Ni vyema kutoa taarifa Tanesco kitengo cha dharura kwa msaada zaidi,”amesema.
Katika hatua nyingine amesema kuwa iwapo mvua itaambatana na
radi upepo mkali au umeme utapungua nguvu na kuongezeka ndani ya nyumba
hivyo wananchi wanashauriwa kuzima umeme kwenye ‘Main switch’, ili
kuepukana na majanga yatokanayo na shoti ya umeme.