Waziri wa Fedha Dr Mpango Awaagiza Wanamipango Kuwezesha Utekelezaji Wa Miradi Ya Ubia Sekta Binafsi Na Umma

Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WFM, DODOMA
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaagiza wataalamu wa mipango nchini kutoa mapendekezo ya kibunifu ambayo yataiwezesha nchi kunufaika na utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP).

Agizo hilo amelitoa wakati akifungua Kongamano la Wanamipango kwa mwaka 2019 lililofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Alisema kuwa bado kunachangamoto ya utekelezaji wa PPP nchini na kuwataka wataalamu hao kujadili ili kuona wapi nchi imekosea na kutoa suluhu ya namna ya kutatua changamoto hizo.

 “Lakini PPP niliyoona imefanikiwa sana ni kwenye sekta za kijamii, najua tumefanya vizuri kwenye huduma za afya na elimu, lakini kweye miradi ya miundombinu bado”, alibainisha.

Aidha, Dkt. Mpango aliwagiza wataalamu hao kujadili namna bora ya kutanua wigo wa kukusanya kodi ili kuiwezesha nchi kuweza kujiendesha pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema katika suala la kodi, ukusanyaji kodi bado kuna shida kwani hata idadi ya walipakodi ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wananchi.

Aliwataka wataalam hao kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji mapato ya Serikali na kuhakikisha yanatumika vema ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.

Aliseme ni vema wataalam hao wakatambua kuwa katika harakati za kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ni wazi baadhi ya vyanzo vya ugharamiaji wa miradi vitapungua hivyo ni lazima nchi iweke mipango madhubuti ya kutafuta rasimali kutoka katika vyanzo mbadala vya mapato za kuweza kugharamia miradi hiyo.

Waziri Mpango alisema kwa kuwa Kongamano hilo linalenga kujadili namna ya kugharamia maendeleo, ni vema wataalamu hao wakajadili na kujatoa muongozo wa namna Tanzania itakavyoweza kuvutia wawekezaji binafsi kwa wingi.

“Ni matarajio ya Serikali kongamano hili litajadili wawekezaji ambao watafanya uwekezaji utakao inufaisha nchi na wao wenyewe, yaani uwekezaji huu uwe ni win-win”, alifafanua.

Aidha, Dkt. Mpango aliwaagiza wataalam hao kujadili namna majukumu ya benki za ndani katika kugharamia miradi ya maendeleo ili kuona namna ya kuzishirikisha katika miradi hiyo.

Naye Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Lorah Madete alisema kuwa kupitia kongamano hilo washiriki watapata fursa ya kujadili mawasilisho yatakayoendana na dhima ya kongamano ikiwemo Vyanzo bunifu vya ugharamiaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, Sera, Sheri ana Kanuni.

Kongamano hilo la siku mbili limekutanisha wataalamu wanaohusika na masuala ya mipango kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi, Sekretariaeti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post