ZIARA YA MAKATIBU WAKUU NGARA MPAKANI MWA TANZANIA NA BURUNDI YAIBUA CHANGAMOTO

Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi, Hamdouny Mansour (mwenye sweta nyeupe) akitoa maelezo kwa wajumbe kuhusu eneo la mpaka linalojulikana kama mafiga matatu (Tanzania, Ruanda na Burundi) katika bonde la Mto Kagera. Kutoka kulia wa Kwanza ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi Bwana Ramadhan Kailima akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti wa nne (mwenye shati la pinki). Kutoka kushoto ni Nicolous Mkapa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi akifuatiwa na Gerald Mweri, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

 
Na Mwandishi wetu

Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya Rais- IKULU, TAMISEMI, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali walifanya ziara Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, kukagau zoezi la uimarishari wa mpaka uliofanyika mwaka 2014.

Ziara hiyo iliyojumuisha wataalam mbalimbali wanaoshughulikia mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na nchi zinazoizunguka, ilikuwa ya siku nne ambapo wajumbe walitembelea baadhi ya maeneo yaliyopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka lililofanyika mwaka 2014.

Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Bwana Florence Turuka ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa wajumbe hao alisema, lengo la kutembelea na kukagua maeneo ya mpaka wa kimataifa uliopitiwa na zoezi la uwekaji wa alama za hifadhi ya mpaka (vigingi) mwaka 2014 ni kukusanya taarifa kutoka kwa wananchi.

Alisisitiza kwamba, taarifa itakayotolewa na wananchi katika maeneo yaliyopitiwa na uimarishaji wa mpaka, itaisaidia Serikali kujua ni mikakati gani iwekwe katika maeneo yanayozunguka mpaka ili kuwalinda wananchi pamoja na mali zao.

Nae mkuu wa Wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mtenjele, alisema katika taarifa ya Wilaya kwamba, mpaka kati ya Tanzania na Burundi uko salama na Wilaya imeendelea kuwa na mahusiano na mawasiliano ya karibu na nchi hiyo. 

Aliongeza kwamba, mara nyingi zinapotokea changamoto mawasiliano ya simu hufanyika na nchi ya Burundi na kuyatatua kitu ambacho kisingewezekana kama mahusiano yangekuwa siyo mazuri.

Taarifa ya Wilaya pia ilibainisha kwamba, zoezi la uimarishaji mpaka lililofanyika mwaka 2014 liliwaathiri baadhi ya wananchi wa Tanzania waliokuwa wanaishi mpakani.

Kanali Michael alisema, pamoja na athari ambazo tayari Wilaya ilishabainisha, wajumbe wanaweza kupata taarifa zaidi kuhusu hali ya mpaka kutoka kwa wananchi wanaoishi mpakani watakapokuwa wanatembelea na kukagua maeneo hayo.

Pamoja na wajumbe kutembelea na kukagua baadhi ya maeneo yaliyopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014, pia walifanya mikutano ya hadhara na wananchi wa vitongoji na vijiji husika ili kupata taarifa ya hali ya mpaka. 

Katika mikutano hiyo ya hadhara, baadhi ya wananchi walisema, zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014 iliwaathiri wao na mali.

Bibi Jesca Lameck mwenye umri kati ya miaka 75-80 ni mmoja kati ya wananchi waliosema zoezi la uimarishaji wa mpaka la mwaka 2014 lilimuathiri. 

Bibi Jesca alisema, katika zoezi hilo lililohusisha uwekaji wa alama (vigingi) katika hifadhi ya mpaka, alijikuta sehemu ya shamba lake la miti, kahawa, matunda na makaburi vikiangukia upande wa nchi ya Burundi.

Baada ya kutembelea na kufanya mikutano na wananchi waliopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014, mwenyekiti Bwana Florence Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi alipokea taarifa kuhusu athari zilizotokana na zoezi hilo, pamoja na changamoto nyingine zinazohusu mpaka tofauti na za uwekaji alama za hifadhi ya mpaka.

Aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Ngara kwa jinsi unavyosimamia mahusiano na nchi ya Burundi na kuahidi  kuifikisha mbele zaidi taarifa aliyoipata kuhusu changamoto za mpaka wa Tanzania na Burundi.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post