Mahakama ya kikatiba ya Malawi imefuta matokeo ya uchaguzi uliomuweka madarakani, Peter Mutharika.
Imesema
uchaguzi huo uliofanyika Mei 21, 2019 haukuwa huru na haki, hivyo
imeamuru urudiwe ndani ya siku 151, mshindi lazima apate kura zaidi ya
nusu ya idadi ya waliopiga kura.
Majaji waliotoa uamuzi huo wakiongozwa na Healey Potani wameeleza
kubaini Tume ya Uchaguzi Malawi (MEC) kupokea ripoti 147 zinazoonyesha
kuwa matokeo hayo hayakuwa sahihi kutokana na kasoro mbalimbali, ikiwa
ni pamoja na baadhi ya matokeo kubadilishwa.
Mutharika alishinda kwa asilimia 38 ya kura zote akifuatiwa na Lazarus
Chakware asilimia 35 na Saulos Chilima aliyewahi kuwa makamu wa rais
ambaye alipata asilimia 20.