Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo
Na Peter Elias, Mwananchi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amesema sampuli
za wanajeshi 10 waliokufa katika mazoezi ya kijeshi zimepelekwa kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.
Mabeyo ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 3, 2020 Ikulu jijini Dar es
Salaam baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha viongozi mbalimbali
aliowateua Januari 31, 2020.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli alitoa pole kutokana
na vifo vya watu 20 katika kongamano wa Nabii na Mtume, Boniface
Mwamposa vilivyotokea mjini Moshi, vifo vya watu 21 mkoani Lindi baada
ya nyumba zao kusombwa na maji na vifo vya wanajeshi hao 10.
Mabeyo amesema wanajeshi hao walikuwa kwenye mazoezi ya kawaida ya kutembea.
Amesema baada ya saa mbili, hali zao zilianza kubadilika wakiwa eneo la Msata, walipelekwa hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Amesema baada ya kulazwa hospitalini hapo, baadhi yao walifariki na
wengine hali zao ziliimarika. Amesema mpaka sasa kuna majeruhi watano.
"Tunahisi walikula chakula chenye sumu, labda wakati wanatembea
walinunua vyakula barabarani vikawadhuru. Mazoezi yalikuwa ya kawaida
tu.”
"Tumepeleka sampuli za waliofariki kwa Mkemia Mkuu ili kubaini chanzo
hasa cha vifo," amesema Mabeyo akizungumzia vifo hivyo vilivyotokea
Januari 30, 2020.