Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Anjela Kairuki, amesema
ofisi yake imepata wawekezaji wakubwa wawili ambao wameonyesha nia ya
kuwekeza katika kilimo ikiwamo kuchakata mafuta ya bangi kwa ajili ya
matibabu.
Kairuki
alikuwa akimpa taarifa mchangiaji aliyekuwa akichangia mjadala wa
taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii,
Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba, aliyetaka serikali
ipitishe jambo hilo mapema kabla bei ya bangi haijaporomoka.
Kishimba wakati anachangia mjadala huo alisema bei ya bangi duniani
imepanda maradufu na nchi zote alizozizunguka wamesharuhusu kilimo cha
zao hilo, hivyo anamwomba Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, atoe
ufafanuzi kwamba watu wanaotaka kulima wamuone nani.
“Waliopiga marufuku bangi ni Wazungu miaka ya 40, lakini Wazungu
walewale waligundua ndani ya bangi kuna dawa, na sisi wenyewe tunaenda
kwenye viwanda vya dawa. Je, sisi tuki- import dawa zenye material ya
bangi (tukiagiza dawa zenye malighafi itokanayo na bangi) tutakuwa
tumeagiza kutoka wapi na tuta declare (kutangaza maslahi) namna gani.
Kwa kuwa bei ya masoko duniani ni bei ya ushindani… ni vizuri serikali
ifanye uamuzi huo mapema zaidi.
Kishimba aliongeza: “Tanzania kwa Afrika ni nchi ya tatu kwa kulima
bangi kwa magendo na kama wataruhusu na sheria kama ilivyo inaweza sana
ikatusaidia kutupeleka mahali. Lakini kwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi (George Simbachawene) yuko hapa anaweza akatoa msamaha hata kwa
bangi iliyokamatwa kwa muda wa miezi sita, kama msamaha anavyoutoa wa
silaha.”
Kwa mujibu wa Kishimba, msamaha huo kama utatolewa na wananchi
wakawasilisha bangi hizo Polisi, watu wakauziana bangi hiyo Polisi na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watapata mapato na wanunuzi wakaja
kununua hapa, linaweza kusaidia wenzetu wakapata pesa na kwa hali hiyo,
lazima tuende haraka sana.
“Uganda wamepewa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), zaidi ya Dola milioni
500 kwa ajili ya kilimo cha bangi, na kwamba kwa kuwa tulianza kulima
bangi muda mrefu, lakini basi namuomba waziri wakati wowote kama
watapitisha iwe mapema kabla bei haijaporomoka,” alisema.
Wakati Kishimba anachangia mjadala huo, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma alisimama na kumpa taarifa akisema:
“Kikawaida Bunge linapotunga sheria kinachofuata ni kanuni tu, sasa
nilikuwa nafikiria Mheshimiwa Waziri angetuambia kanuni ziko tayari ili
tuanze kulima kwa sababu bangi itaporomoka bei.”
Baada ya michango hiyo ya wabunge, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema:
“Niwa assue this is not a joke (niwahakikishie kwamba hili sio jambo la
utani), anachochangia (Kishimba)… nilikuwa Canada majuzi hapa kwenye
mkutano wa ma Spika wa Common Wealth (Jumuiya ya Madola) duniani. Ni big
business in Canada (Ni biashara kubwa). Kwa hiyo anazungumza kitu cha
msingi sana wala sio utani.
“Tena linaweza kuwa ni zao kubwa la biashara linaoweza kundoka kuliko
mazao mengi tu kabisa, likafanya mapinduzi makubwa sana ya kipato. Kwa
hiyo anachokizungumza Mheshimiwa Kishimba hazungumzi bangi itumike vile
ambavyo tunavyofahamu inatumika hapa nchini.
“Tunazungumzia habari ya kilimo, moderated, monitored na taratibu zote
halafu wanapelekewa wote wanaohitaji kwa ajili ya kutengeneza dawa za
wanyama na binadamu.”