Na James K. Mwanamyoto - Mpwapwa
Taasisi za Kifedha nchini, zimeithibitishia Serikali
kutoa mikopo kupitia Hatimiliki za Kimila zinazotolewa na Mpango wa Kurasimisha
Rasilimali na Biashara za Wanyonge
Tanzania (MKURABITA) ili kuwawezesha wananchi waliopatiwa hati hizo
kuboresha maisha yao.
Akizungumza katika Kijiji cha Inzomvu Wilayani Mpwapwa
jana kwa niaba ya Taasisi za Kifedha nchini, Meneja wa NMB Tawi la Mpwapwa, Bi. Beatrice Mwasa amemthibitishia Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) kuwa taasisi
hizo ziko tayari kuwakopesha wananchi ili kuunga mkono jitihada za maendeleo
zinazofanywa na wananchi kupitia hati hizo.
Bi. Mwasa amesema, Taasisi hizo za Kifedha zinatoa mikopo
kwa shughuli za kibiashara na kilimo kwa maeneo yaliyoendelezwa na mpaka sasa
zimemeshatoa mikopo zaidi ya 100 kwa wananchi wa Mpwapwa na wako tayari
kuendelea kutoa mikopo kwa wananchi wengine watakaopata hati hizo.
Bi Mwasa ameziainisha Taasisi zilizotoa mikopo hiyo kwa
wananchi kuwa ni NMB, CRDB, Benki ya Posta na FINCA, hivyo amewataka wananchi
wenye hati hizo kutumia fursa hiyo kujiendeleza kimaisha.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika amezishukuru
taasisi hizo kwa kukubali kutoa mikopo kupitia Hatimiliki za Kimila tofauti na
ilivyokuwa hapo awali.
Mhe. Mkuchika amesema, awali Serikali ilikuwa
ikilalamikiwa kuwa Taasisi za Kifedha hazitambui Hatimiliki za Kimila lakini
hivi sasa zimeungana na Serikali kuboresha maisha ya watu wenye kipato cha
chini.
Mhe. Mkuchika amewataka Wananchi wanaokopa kupitia
Hatimiliki za Kimila kutumia mikopo hiyo vizuri katika masuala ya maendeleo na
sio vinginevyo ili waweze kuirejesha na kuwawezesha wengine kupata ili kuinua
uchumi wao.
Akiwa
katika ziara kikazi ya kukagua utekelezaji wa MKURABITA Wilayani Mpwapwa jana, Mhe.
Mkuchika alitoa jumla ya Hatimiliki za Kimila 10 kwa niaba ya Wanakijiji 159 wa
Kijiji cha Inzomvu Wilayani Mpwapwa.
Kwa
upande wake, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amesema jumla ya Hatimiliki
za Kimila 593 zilitakiwa kutolewa lakini kutokana na changamoto za kiutendaji
zimetolewa Hatimiliki 159.