Wakandarasi mradi wa Maji Tabora watakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji

Na Mwandishi Wetu,Tabora
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amewataka wakandarasi wanaojenga mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega, Uyui na Tabora kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili ukamilike kwa wakati.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akikagua na kutoa maelekezo ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akipokea maelezo ya ujenzi wa mradi kutoka kwa Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui wakati wa ziara yake kwenye mradi huo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akitoa maelekezo kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui wakati wa ziara yake kwenye mradi huo.
Ujenzi ukiendelea kwenye moja ya eneo la mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui

Mhandisi Sanga ametoa maelekeo hayo Mkoani Tabora Februari 4, 2020 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji mkoani humo.

Mara baada ya kutembelea eneo la mradi huo na kujionea hatua iliyofikiwa, Mhandisi Sanga alizungumza na wakandarasi wanaoutekeleza ambapo alieleza kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa. 

Hata hivyo, licha ya kuridhishwa na ubora wa ujenzi wa mradi, Mhandisi Sanga aliwataka wakandarasi hao kuelekeza nguvu zaidi kwenye kazi zinazopelekea wananchi kupata maji kwanza badala ya kuweka nguvu kubwa kwenye maeneo mengine.

“Pamoja na kazi nzuri inayoonekana kufanyika maaelekezo yangu ni kuwa wakandarasi wote mhakikishe kuwa kazi zinazofanyika kwa sasa ni zile ambazo wananchi wataanza kupata maji mapema iwezekanvyo badala ya kuweka nguvu kwenye majengo na mambo mengine,“ alisisitiza Mhandisi Sanga. 

Alibainisha kuwa wananchi wamesubiri mradi huo kwa muda mrefu na kwamba kwakuwa tayari kumefanyika kazi kubwa wahakikishe maeneo machache ambayo bado hayajakamilika wanayakamilisha. 

“Mnapaswa kuelewa wananchi wameusubiri mradi huu kwa muda mrefu, hizi kazi zilizobakia mhakikishe zinakamilika haraka, shughuli zingine kama kupaka rangi majengo zitafanyika baada ya kuwa tayari wananchi wanapata huduma,” aliongeza Mhandisi Sanga. 

Kwa upande wao Wakandarasi hao walimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kutekeleza maelekezo aliyoyatoa na waliahidi kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi wa mradi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hadi muda wa ziada ili tu inapofika Februari mwishoni maji yawe yamefika kwenye maeneo yote yaliyokusudiwa ya Tabora mjini, Nzega, Igunga na Uyui.

Mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui unajengwa na Kampuni tatu kutoka India ambazo ni Megha Engineering Infrastructures, L&T na Afcons kwa gharama ya shilingi  Bilioni 602 zikiwa ni fedha za mkopo kutoka benki ya Exim ya India. 

Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kutoka Agosti 2017 na unatakiwa kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 kwa mujibu wa mkataba na kwamba kukamilika kwake kutawezesha jumla ya wananchi 1,200,000 kunufaika na huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post