WANANCHI WATAKIWA KUCHANGIA SEKTA YA ELIMU KAHAMA

Mwalimu Bukuru Robert wa shule ya Msingi Mtakuja akiwafundisha wanafunzi wa darasa la pili somo la Kiswahili katika darasa ambalo linawanafunzi zaidi ya 50 huku wengine wakiwa wamekaa chini kwa kukosa madawati.
Na Salvatory Ntandu - Kahama
Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na madawati katika shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, jamii imetakiwa kuchangia shughuli za maendeleo hususani sekta ya elimu ili kutatua kero hiyo inayosababisha wanafunzi kukosa masomo.
Wito huo umetolewa Febuari 3,2020 na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Thomas Myonga katika ziara ya siku mmoja ya kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na halmashauri hiyo katika kipindi cha miaka mine ya serikali ya awamu ya Tano.
Alisema tatizo la wanafunzi kukosa vyumba vya madarasa na madawati linachangiwa na wananchi kutochangia shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo na madawati jambo ambali linasababisha wanafunzi kushindwa kusoma vizuri.
“Nimetembelea shule ya msingi mtakuja yenye wanafunzi 2467 yenye vyumba vya madarasa 12 ambayo hayatoshi na baadhi ya wanafunzi wanasomea wakiwa wamekaa chini nimebaini wazazi na wananchi wa eneo hili hawajachangia ujenzi wa madarasa”,alisema Myonga.
Myonga aliwataka wakazi wa mtaa wa mtakuja na kata ya Nyahanga kuchangia ujenzi wa madarasa pamoja na madawati ili kuondoa tatizo la wanafunzi kusomea wakiwa wamekaa chini sambamba na kusoma kwa awamu jambo ambalo linasababisha washindwe kufanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba  aliwataka watendaji wa kata mitaa na vijiji kuwahamsisha wananchi kujenga maboma ya madarasa katika maeneo ambayo yanachangamoto ili halmashauri iweze kuyakamilisha na kuondoa tatizo hilo.
“Viongozi wa serikali za mitaa na vijiji shirikianeni na wataalamu wangu kuhamasisha wananchi kuchangia katika sekta ya elimu ili kuondoa changamoto zinazowakabili wanafunzi wetu kwa kukosa vyumba vya madarasa,madawati na matundu ya vyoo”,alisema Msumba.
Alisema mwitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi shule umekuwa mkubwa baada ya serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne na kusababisha shule nyingi kukabiliwa na changamoto hizo.
Kamati ya siasa ya wilaya ya Kahama inaendelea na ziara ya siku mbili katika halmashauri ya Mji wa kahama katika utekelezaji ilani ya CCM sambamba na Maadhimisho ya miaka 43 ya CCM yanakwenda na kauli mbiu isemayo “tumeahidi,tumetekeleza na tunaahidi tena kuchapa kazi kwa juhudi,ubunifu na maarifa zaidi”.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post