MKOA
wa Lindi kihistoria sio wa kiufugaji ma wafugaji wachache waliopo
hufuga zaidi mbuzi, kondoo, kuku, bata, kanga, njiwa na ng’ombe ambao
kwa uchache sana na mara nyingi hutumiwa kwa kitoweo, shughuli za
biashara, kimila na utamaduni.
Mara
baada ya baada ya Serikali ya Mkoa huo kukubali kupokea mifugo toka
Mikoa mingine yenye idadi kubwa ya ng’ombe, sekta ya mifugo imeendelea
kukua na kuongeza mwamko kwa wananchi katika kujiletea maendeleo yao.
Mkoa
wa Lindi hadi kufikia mwezi Machi, 2018 una jumla ya ng’ombe wa asili
118,760, mbuzi asili 79,183, mbuzi wa kisasa 8,138, na kondoo 9,007,
ngamia 10, Nguruwe 5,166, kuku 1,460,491, punda 121, kanga 5,788, bata
maji 25,111, bata mzingi 112, Njiwa 1,586 na Sungura 212.
Kwa
mujibu wa Taarifa ya Mkoa, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi
2018 fedha zilizotokana na biashara ya mifugo katika Halmashauri zote
mkoani humo zilikuwa ni zaidi ya Tsh. Bilioni 5.1 zilizotokana na ushuru
wa machinjio, leseni za wafanyabiashara wa nyama pamoja na usafirishaji
wa mifugo.
Pamoja
na sekta hiyo kuwa chanzo muhimu cha mapato katika Mkoa huo, bado kuna
msukumo mdogo wa Serikali katika uendelezaji wa miundo mbinu ya mifugo
ikiwemo machinjio, maeneo kwa ajili ya malisho, maeneo ya malambo kwa
ajili ya mifugo, majosho pamoja na uchache wa mashamba ya mifugo.
Katika
kukabiliana na changamoto hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi
inatekeleza ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa katika eneo la Ngongo
unaolenga katika kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ikiwemo nyama
ambayo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku mkoani humo.
Halmashauri
hiyo hadi sasa imetumia kiasi cha Tsh Bilioni 1.4 zilitolewa na
Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha mradi huo, ambao ni moja ya miradi
ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri hiyo ili kuiwezesha
kujitegemea kimapato katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi.
Akizungumza
katika mahojiano maalum na Maafisa kutoka Idara ya Habari (MAELEZO)
waliofanya ziara hivi karibuni Mkoani humo, Mhandisi Godfey Msoma wa
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, anasema mradi huo ulioanza mwaka 2017
umekamilika kwa asilimia 98, ikiwemo awamu muhimu mbili za mwanzo
zinazohusisha jengo la machinjio pamoja na miundombinu yake.
Anaongeza
kuwa mradi wa machinjio hayo pindi utakapokamilika utaweza kutoa huduma
ya kuchinja ng’ombe 100, mbuzi 100 kwa siku na hivyo kufungua milango
ya uwekezaji mkubwa na wenye tija kwa kwa wafugaji na wafanyabiashara
mkoani huo pamoja na Mikoa jirani katika Ukanda wa Kusini.
‘’Kwa
Manispaa ya Lindi, hii ni fursa na tutatumia mradi huu kwa ajili ya
kuhamasisha wananchi wetu wafuge kisasa kwani kwa kufanya hivyo
kutawawezesha kujiongezea fursa ya masoko kwa mifugo yao na kuweza
kufanya minada ya mifugo yao na pia kuuza bidhaa za nyama zenye ubora
wa kimataifa’’ alisema Msoma.
Aidha
Msoma alisema malengo ya ujenzi wa mradi huo ambao pia ni miongoni mwa
miradi mikubwa ya uwekezaji katika Halmashauri hiyo ni kukidhi mahitaji
makubwa ya machinjio ya kisasa katika Ukanda wa Kusini kutokana na
ukweli kuwa mikoa hiyo kwa sasa inaendelea kupokea makundi makubwa ya
wafugaji wa kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Kwa
mujibu wa Msoma alisema ili kuhakikisha machinjio hayo yanakuwa ya
kisasa na endelevu, mradi huo pia utahusisha ujenzi wa nyumba ya Daktari
wa wanyama ambaye atakuwa na jukumu la kufanya ukaguzi na uhakiki wa
ubora wa nyama inayozalishwa kabla ya kumfikia mlaji ili kuhakikisha
kuwa afya za walaji zinalindwa kwa manufaa ya jamii husika.
‘’Machinjio
haya ni ya kisasa kabisa katika ukanda wa kusini, malengo yetu ni
kuhakikisha tunakidhi viwango vya kimataifa katika uzalishaji wa nyama
bora ili kuweza kupanua mahitaji ya soko la bidhaa za nyama kimkoa,
kitaifa na kimataifa, hivyo tumepanga kuhakikisha kuwa miundombinu yake
inakuwa na sifa zinazostahiki’’ alisema Msoma.
Kwa
upande wake Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri hiyo,
Dkt. Iddi Nizari ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa kiasi
kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambao umejengwa
katika viwango vya kimataifa kwa kuwa utasaidia kuongeza mapato ya Mkoa
wa Lindi na taifa kwa ujumla.
Aliongeza
kuwa ujenzi wa mradi wa machinjio hayo unatarajia kuongeza chachu ya
uwekezaji kwa wafugaji na wafanyabiashara wa nyama mkoani humo kwani
utaweza kuhudumia wanyama wengi na hivyo kutoa fursa ya kufanyika kwa
minada mikubwa katika Ukanda wa Kusini.
‘’Machinjio
haya yatazalisha nyama bora zinazouzwa katika maduka mbalimbali na pia
kupanua soko letu la nyama katika nchi za nje kwani watumaji wengi wa
nyama waliopo nje ya nchi wanaopenda kuona bidhaa iliyozalishwa katika
viwango vyenye ubora na hili kwa upande tumejipanga katika kufikia
viwango hivyo’’ alisema Dkt. Nizari.
Akifafanua
zaidi Dkt. Nizari alisema ujenzi wa machinjio hayo utasaidia kutoa
hamasa kwa wafugaji mkoani humo kufuga kisasa zaidi hatua itakayowezesha
kuongeza tija ya uzalishaji wa bidhaa ya nyama mkoani humo kuweza
kufikia mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
‘’Machinjio
tunayoitumia sasa ni ndogo sana lakini pia haina ubora wa kuhudumia
mifugo yetu kwa mfano machinjio tunayoitumia kwa sasa katika Halmashauri
yetu ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 10 na mbuzi 20 kwa siku, hivyo bado
hatujaweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika Halmashauri’’ alisema
Dkt. Nizari.
Aidha
Wananchi mbalimbali katika Manispaa ya Lindi walitoa pongezi kwa
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa
ujenzi wa mradi huo, ambao wanaueleza utakuwa mkombozi kwa wananchi wa
mikoa ya Kanda ya Kusini kwani utafungua milango ya kiuchumi na
kuimarisha sekta ya mifugo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Mmoja
wa Wananchi wa Kata ya Tulieni, Manispaa ya Lindi Bw. Bakari Mchukuma
anasema ujenzi wa machinjio ya kisasa utasaidia kuondokana na ufugaji wa
kimazoea kwani hapo awali walikuwa na mifugo mingi katika jamii yao
ikiwemo ng’ombe ambao wilitumika katika shughuli mbalimbali za kimila
ikiwemo ngoma za asili zinazofanyika kila mwaka mara baada ya kumalizika
kwa msimu wa kilimo.
‘’Mkoa
wetu haukuwa mkoa wa kifugaji, tulikuwa na ng’ombe, Mbuzi, kondoo, kuku
na mifugo mingine ambayo mingi ilitumika kwa ajili ya sherehe za kimila
ikiwemo ngoma, lakini kwa sasa Serikali ya Rais Dkt. John Maguful
imeamua kujenga machinjio kubwa, bora ya kisasa katika manispaa ya
Lindi, ambayo itatusaidia kuiuza na kupata pesa kwa ajili ya kuendesha
maisha yetu’’ anasema Mchukuma.
Aidha
Mchukuma aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa mradi huo
kwani utasaidia kuongeza idadi ya minada ya mifugo Mkoani humo, ambapo
kwa sasa kuna jumla ya minada minne tu ambapo kati ya hiyo, minada
miwili inapatikana Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mnada mmoja uliopo
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi huku Halmashauri ya Lindi pia ikiwa na
mnada mmoja.
Kwa
upande wake Bw. Abdul Kasembe Mkazi wa kijiji cha Mitandi Manispaa ya
Lindi, ambaye ni mfugaji anayemiliki ng’ombe 30, mbuzi 45 na kondoo 25,
aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa mradi wa machinjio
hayo kwa kuwa umedhihirisha dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli ya
kusaidia wananchi wa kipato cha chini katika kujikwamua kiuchumi.
Anaongeza
kuwa kwa upande wake machinjio hayo yamempa fursa ya kufuga kisasa,
kwani ataweza kuiuza mifugo yake katika minada mikubwa inayotambulika na
Serikali na kuwasaidia kulanguliwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Naye
Bw. Emmanuel Kwaang, mkazi wa kijiji cha Matopeni Manispaa ya Lindi
ambaye pia ni mfugaji wa mbuzi na kondoo anasema uwepo wa machinjio hayo
utasaidia kupatikana kwa soko la uhakika wa mifugo mkoani humo,
ukilinganisha na hali ilikuwapo hapo awali ambapo walikuwa wakisafiri
hadi mikoa ya jirani ikiwemo Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kutafuta masoko.
Bw.
Kwaang aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha kwa ajili
ya ujenzi wa mradi huo kwa kuwa utasaidia upatikanaji wa masoko ya
uhakika wa mifugo yao sambamba na kupunguza umbali wa kusafirisha mifugo
yao, ambayo hupungua thamani pindi wanapoenda kuiuza katika minada
iliyopo nje ya Mkoa huo.
‘’Nampongeza
Rais Dkt. John Magufuli kupitia Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa
machinjio haya kwani imetusaidia sana sisi wafugaji kuweza kupata soko
la uhakika la kuuzia mifugo yetu na hivyo kuweza kuchangia pato la Mkoa
wetu wa Lindi kutokana na Kodi tutakayoanza kuilipa pindi machinjio haya
yatakapoanza kufanya kazi’’ alisema Kwaang.
Naye
Bw. Hamis Mohamed mfanyabiashara wa bidhaa za nyama na Mkazi wa RahaLeo
Manispaa ya Lindi, anasema ujenzi wa machinjio hiyo utawasaidia
kuongeza wigo wa biashara yake Mkoani humo na mikoa ya jirani kutokana
na ubora wa nyama itakayozalishwa kiwandani hapo kuwa ni yenye ubora na
hivyo kufungua milango ya ushirikiano wa biashara baina ya Tanzania na
nchi jirani ikiwemo Msumbiji.
‘’Pindi
machinjio haya yakikamilika na kuanza kazi yatasaidia kupanua mtandao
wa biashara baina yetu na mataifa jirani ikiwemo nchi ya Msumbiji, na
kufanya hivi kutasaidia kuongeza kodi ya serikali naipongeza serikali ya
Awamu ya Tano kwa kubuni mradi huu ambapo utafungua fursa ya ukuaji wa
biashara kwa mikoa ya ukanda wa kusini’’ alisema Mohamed.
Serikali
kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
inatekeleza Mkakati Maalum unaolenga kuziwezesha Mamlaka za Serikali za
Mitaa ikiwemo Halmashauri kujitegemea kimapato ili kutoa huduma bora
zaidi na zenye uhakika kwa wananchi.
Kwa
kuzingatia sababu hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha utaratibu
kwa Halmashauri mbalimbali nchini kufanya mawasilisho ya miradi yao ya
kimkakati katika eneo la kujijenga kimapato kwa madhumuni ya kujitegemea
na kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa
msingi huo, ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Halmashauri ya
Manispaa ya Lindi utasaidia upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye
uhakika katika Halmashauri hiyo ikiwa ni nguzo imara katika kuboresha
utoaji huduma nzuri na zenye uhakika kwa wananchi.