Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto)
akimkabidhi Cheti cha Ushindi Meneja Utawala na Rasilimali Watu wa MWAUWASA,
Deogratius Magayane mara baada ya hafla.
|
Cheti cha ushindi kilichokbidhiwa kwa MWAUWASA
|
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (aliyesimama) akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Cheti cha Ushindi kutoka EWURA |
Mamlaka
ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imetunukiwa cheti
cha ushindi wa tatu katika utoaji wa huduma nzuri za majisafi na usafi wa
mazingira kwa Mwaka 2018/19 katika kundi la Mamlaka za Maji za Mikoa.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Ewura ya Mwaka 2018/19, Mamlaka za Maji za Mikoa
zilizoibuka kinara katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira ni
Mamlaka ya Maji Moshi ambayo imeshika nafasi ya kwanza, Mamlaka ya Maji Iringa
ambayo imeshika nafasi ya pili na Mamlaka ya Maji Mwanza ambayo imeshika nafasi
ya tatu.
Akizungumza
Ofisini kwake Jijini Mwanza Mei 13, 2020 wakati wa hafla ya utoaji wa cheti kwa
MWAUWASA, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
Kanda ya Ziwa, George Mhina alisema uzinduzi wa taarifa za Mamlaka za Wilaya na
Miji na ile ya Mamlaka za Mikoa na Miradi ya Kitaifa ulikuwa ufanyike Dar es
Salaam hata hivyo alisema haukuweza kufanyika kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa
Corona (COVID 19).
“Katika
kuchukua tahadhari dhidi ya COVID-19 na ili kuepuka mikusanyiko ya watu wengi;
iliamuliwa Mamlaka zilizofanya vizuri zipokee tuzo na vyeti kupitia ofisi za
kanda za EWURA nchini kote tofauti na ilivyokuwa inafanyika katika miaka
iliyopita kwa viongozi wa Mamlaka za Maji zote kukutana kwenye mkutano wa
pamoja wa mwaka,” alifafanua Mhina.
Mhina
alivitaja vigezo vilivyotumika kushindanisha Mamlaka za Maji kuwa ni kiwango
cha maji yanayozalishwa, idadi ya wananchi wanaopata huduma, ubora wa maji,
idadi ya wateja wa huduma ya majisafi na mtandao wa uondoshaji majitaka, uwiano
wa watumishi na idadi ya wateja sambamba na ufanisi wa ukusanyaji wa maduhuli.
Aidha,
Mhina aliipongeza MWAUWASA kwa kushika nafasi hiyo ya tatu kati ya Mamlaka 26
zinazotoa huduma kwenye Makao Makuu ya Miji Mikuu ya Mikoa.
Akielezea
taarifa ya Ewura 2018/19 Mhina alisema inadhihirisha Mamlaka za Maji
zinaendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na taarifa za kipindi cha nyuma huku
akitolea mfano maeneo ambayo Mamlaka zimeongeza ufanisi ikiwemo kuongezeka kwa
kiwango cha maji yanayozalishwa, kuongezeka kwa idadi ya wateja na kuimarika
kwa ubora wa maji.
Mhina
alisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa mafanikio yaliyoonyeshwa na Mamlaka nyingi
za maji zipo changamoto zinazohitaji ufuatiliajia wa karibu zaidi ambazo ni
pamoja na upotevu mkubwa wa maji, kukosekana kwa mifumo ya majitaka kwenye
baadhi ya mamlaka na changamoto ya weledi miongoni mwa baadhi ya wataalam
kwenye baadhi ya Mamlaka.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele
wakati akipokea cheti aliishukuru EWURA kwa mwongozo juu ya namna ya kuboresha
upatikanaji wa huduma na aliahidi kufanya vizuri zaidi.
“Tunashukuru
kwa kupata ushindi huu lakini tunaahidi kuongeza jitihada kwenye utendaji wetu
wa kila siku ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwenye maeneo
tunayoyasimamia,” alisema Mhandisi Msenyele.