***********************************
Na WAMJW – Dar es Salaam
05/05/2020 Waandishi wa Habari
nchi wametakiwa kuandika habari sahihi kuhusu virusi vinavyosababisha
ugonjwa wa Corona (COVID-19) ili wananchi wapate taarifa ambazo
zitawasaidia kujikinga na ugonjwa huo.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar
es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa vifaa kinga,vifaa vya kupima
joto la mwili, vipeperushi, mabango na vifaa vya kutoa elimu kwa Umma
kwa ajili ya waandishi wa Habari vilivyotolewa na Shirika la UNESCO.
Waziri Ummy alisema wizara yake
imekuwa ikishirikiana na vyombo vya habari kuhakikisha wananchi
wanapata taarifa kwa wakati kuhusu ugonjwa wa Corona na kufahamu hatua
za kufuata ili wajikinge na ugonjwa huo.
“Msaada huu unagusa wadau muhimu
sana kwani hawa ndiyo wanaotusaidia kupeleka taarifa kwa wananchi.
Mmenifurahisha zaidi kuzifikia redio za jamii 34 ambazo zitapata vifaa
vya kupima joto la mwili pamoja na vifaa kinga vingine. Redio hizi ni za
muhimu sana kwani zinawafikia wananchi wengi waliopo vijijini”,.
“Kwa upande wa waandishi wa
habari , pamoja na majukumu yenu ya kazi za kila siku mnazozifanya
hakikisheni mnatoa taarifa sahihi za Corona na siyo habari za kuwatisha
wananchi bali waelimisheni. Nanyi hakikisheni mnafuata maelekezo
yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na ugonjwa huu hii
ikiwa ni pamoja na kusimama umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na
mtu wakati mnapotekeleza majukumu yenu”, alisema Waziri Ummy.
Akikabidhi vifaa hivyo mwakilishi
mkazi wa Shirika la UNESCO Tanzania Tirso Dos Santos aliipongeza
Serikali kwa hatua zinazochukuwa katika kupambana na ugonjwa wa Corona.
“Vyombo vya habari vimekuwa mstari
wa mbele katika kutoa taarifa za ugonjwa huu kwa wananchi, nasi tumeona
tuwape vifaa kinga, mabango na vipeperushi ambavyo zitawasaidia
kuufahamu zaidi ugonjwa wa Corona na kufikisha taarifa sahihi kwa
wananchi kwa wakati”, alisema Santos.
Vifaa vilivyotolewa na Shirika la
UNESCO ambavyo vitatolewa kwa waandishi wa habari ni vitakasa mikono,
barakoa, mashine za kupima joto la mwili, mabango na vipeperushi.