CORONA YAIFUNDISHA JAMII NIDHAMU YA USAFI

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Licha ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) kuleta taharuki katika jamii lakini kwa upande mwingine imesaidia kuielimisha jamii umuhimu wa usafi kama vile kunawa mikono kila mara ikiwa ni pamoja na kutogusana kiholela.

Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya wakazi wa mji wa Arusha walipozungumza na APC Blog juu ya athari ya ugonjwa huo ambapo walisema licha ya kuwa ulileta taharuki katika jamii lakini umesaidia kutoa elimu ya afya ambayo wataendelea kuizingatia siku zote.

“Kwa kweli tulizoea kuishi maisha ambayo kiafya hayakuwa salama, kumbe hatupaswi kushikana mikono, kupiga chafya au kukohoa bila kuziba mdomo kwa mitambaa au mikono, lakini pia tulikuwa hatufahamu kama misongamano siyo salama kiafya” Alisema mama Vivian mfanyabiashara wa chakula maarufu kama ntilie katika soko la Mbauda.

“Mfano kama mteja anakula chakula ambacho haitaji kutumia mikono tulikuwa tunampatia kijiko anaendelea kula, lakini kwa sasa uwe unakula kwa kijiko, mkono au unataka tu kuingia ndani kuulizia bei ya chakula, ni lazima unawe kwenye ndoo hiyo hapo nje ndo uingine ndani uhudumiwe” Aliongeza

Kwa upande wa wauza nguo za mitumba katika eneo la Manzese nao wamesema wanahakikisha kila mteja anayefika eneo la baishara zao wanampa dawa ya kutakasa mikono (sanitizer) ndiyo aendelee kuchagua nguo.

Mmoja wa wafanya biashara wa nguo hizo za mitumba Abdul Komu amesema hali hiyo itakuwa endelevu kwani wameshajua umuhimu wa afya kwa kuwa inawasaidia kuwakinga na magonjwa mengi tofauti na CORONA.

APC Blog imeshuhudia maafisa afya kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji wakipita katika kituo cha daladala Kilombero na kutoa elimu ya unawaji wa mikono hasa kwa abiria wanaotumia usafiri huo kuhakikisha hawapandi bila kuna mikono.

“Hakikisheni kila daladala mnayopanda mnapewa maji ya kunawa au kitakasa mikono, sisi maafisa afya tumetoa dawa ya kuweka kwenye maji kwa kila gari, kwa hiyo msiogope mkasema mbona haya maji hayana sabuni. Hivyo hakikisheni mnatunza afya zenu kwa hiari msisubiri kulazimishwa” Alisema mmoja wa maafisa afya ambaye alisema hawezi kutaja jina lake kwa kuwa yeye siyo msemaji wa suala hilo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post