WAAMUZI WA SOKA WENYE MAAMUZI YA KUPONGEZWA, HAWA HAPA.


Mara nyingi, viongozi wa klabu nyingi za soka katika madaraja tofauti, hasa hapa nchini, mashabiki, wadau na wakati fulani hata wachezaji wenyewe, wamekuwa wakiwalaumu na kuwalalamikia sana waamuzi, kila mmoja akilalama anavyoona inamfaa, hususani timu yake inapopata matokeo hasi.


Wapo ambao wamekuwa wakidai uwezo wa baadhi ya waamuzi ni mdogo katika kuzitafsiri sheria, wengine wakidai wanafanya makusudi kwa sababu fulani fulani hivi, kuipendelea timu moja na nyingine kuionea,  lakini wengine wakidai wanafanya hivyo kwa maelekezo, sitaki kuamini moja kwa moja madai hayo, wala kupingana nayo,  japo nami kwa wakati fulani, kwa sababu pengine tofauti na wengine, nimekuwa nikifanya hivyo.


Katika ubinadamu wao, waamuzi nao wanaweza kukosea kama binadamu mwingine yeyote yule, iwe ni kwa kutokujua kwa kupitiwa au kwa makusudi, ni binadamu,  na binadamu ndivyo tulivyo, hatujakamilika kwa kila jambo, yaani, siyo rahisi, binadamu kufurahiwa na kila binadamu mwenzake kwa kila analolitenda.


Kinachoniumiza moyo, kunitesa nafsi na kunisikitisha, ni ugumu wa binadamu, nadhani kwa ugumu wa mioyo yetu, kushindwa kukubali na kupongeza kazi ya binadamu mwenzake pale anapokuwa amefanya vizuri, nadhani pia, karoho ka wivu kanatutesa na kutusumbua.


Walisema wahenga, nasi hatuna budi kusema, mnyonge, mnyongeni, lakini haki yake apewe.


Tunapowalaumu waamuzi wa soka letu, pale tunapodhani wamekosea, tuwapongeze na kuwashukuru pale tunapokiri wamefanya vyema.


Binafsi nimekuwa na sifa hizo, ninapenda na huwa nafurahi sana kumpongeza yeyote anayefanya vizuri katika kazi aliyotakiwa kuifanya.


Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL) 2020/21, tangu ianze, ipo katika mzunguko wa tisa, tumeshuhudia mara kibao, waamuzi baadhi wakilaumiwa na baadhi ya watu wa mpira wa miguu, kwamba hawatendi haki katika maamuzi yao, lakini, sijawahi kusikia waamuzi wetu wanaofanya vizuri wakipongezwa kwa kufanya vizuri, kama kwamba awapo wanaofanya vizuri, hivi kweli, hakuna waamuzi wanaofanya vizuri, mbona hatuwapongezi, kwa nini hatuwapongezi!


Napenda niwe wa kwanza msimu huu wa ligi, kuwapongeza waamuzi ambao, binafsi mpaka kufikia mzunguko wa tisa, wamenivutia kwa kazi yao nzuri, kama ligi ingeisha leo, hao kwangu wangekuwa waamuzi bora, na pengine kustahili kupewa tuzo kwa kazi nzuri na uwezo wao mkubwa wa kuzitafsiri sheria 17 za mpira wa miguu. 


Niwapongeze na kuwasifu sana, waamuzi waliochezesha mchezo kati ya Mwadui FC na Ruvu Shooting,  uliochezwa November 4, 2020 katika uwanja wa Mwadui complex,  Mwadui,  Shinyanga. 


Mwamuzi wa katikati Martin Saanya, akisaidiwa na Joseph Masija (L1) na Leornad Mkumbo (L2), waliochezesha mchezo huo, (Mwadui  Fc Vs Ruvu Shooting)ni waamuzi ambao wana viwango,  ubora na sifa kedekede za kuchezesha mpira wa miguu.


Waamuzi hao, kwa namna walivyochezesha mchezo huo, hata wakiteuliwa kuchezesha fainali za kombe la Dunia, nina imani na hakika, watafanya vizuri, kupitia wao, waamuzi wetu wataaminika Kimataifa, na kuijengea heshima nchi yetu katika ulimwengu wa soka.


Saanya na wasaidizi wake katika mchezo huo, wameonesha uwezo, wanaweza kuzitafsiri sheria katika kiwango cha hali ya juu mmo, wanastahili pongezi na tuzo kwa kazi nzuri wanayoifanya. 


Waamuzi hawa kwa kazi nzuri waliyoifanya katika mchezo huo, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, waendelee kuwa kielelezo na mfano bora kwa wengine katika katika kuzitafsiri kwa weledi, sheria 17 za mpira wa miguu.


Lakini pia, nimshukuru na kumpongeza sana Kamishina wa mchezo huo, Mwl Zainabu Hassan, ambaye, mbali na kuwaongoza vyema waamuzi hao, uongozi wa Ruvu Shooting,  umetambua uwezo wa kipekee alionao katika kusimamia mpira, ni mama mtu wa mpira, anao uwezo mkubwa wa kuongoza na kuusimamia mpira,  ni mmoja wa makamishina wenye uwezo na weledi katika kutekeleza majukumu ya kazi yake hiyo.


Nimalize kwa kusema kwamba, mpaka sasa, waamuzi wangu bora wa msimu huu wa ligi ni Marrin Saanya, Joseph Masija na Leornad Mkumbo. Mungu azidi kuwasimamia,  waendelee kuifanya kazi hii kwa weledi mkubwa.


Ameandika, Masau Kuliga Bwire  - Mzalendo. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post