AtoZ YATUNUKIWA TUZO YA UBORA NA OSHA

Egidia Vedasto

Arusha

Kiwanda maarufu cha uzalishaji wa chandarua chenye dawa ya kuzuia Mbu wanaoeneza Malaria, nguo na vifaa vya nyumbani cha AtoZ cha Jijini Arusha  kimetunukiwa  Tuzo ya Mazingira Bora mahali pa kazi kutoka katika Taasisi ya Kiserikali inayosimamia Usalama wa Wafanyakazi Mahali pa kazi (OSHA).

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea Tuzo hiyo usiku wa kuamkia Mei Mosi mwaka huu Jijini hapa, Meneja Usalama na Mazingira wa Kiwanda hicho Mhandisi Harrison Rwehumbiza amesema ushindi huo unatokana na uongozi wa kiwanda kuweka mazingira bora na salama kwa wafanyakazi wake.

Hata hivyo pamoja na Tuzo hiyo, Mhandisi Rwehumbiza ameendelea kuwasisitiza  wafanyakazi wa kiwanda hicho kutumia vifaa vya kujikinga wanapokuwa kazini ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

AtoZ ni miongoni mwa viwanda vichache nchini na Afrika vilivyoajiri zaidi ya Wafanyakazi 8000 wengi wao wakiwa ni Wanawake.

Mhandisi Harrison Rwehumbiza akiwa ameshikilia Tuzo ya ubora wa usalama mahali pa Kazi, kutoka OSHA

"Nimekuwa nikiwasisitiza wafanyakazi wasiweke vifaa vya kujikinga na hatari  kwenye begi wawapo kazini kwani vina umuhimu mkubwa katika kulinda afya zao" amesema Rwehumbiza na kuongeza:

"Tunajitahidi sana kuweka mazingira bora na salama  kwa wafanyakazi wetu, na ndio maana leo Taasisi ya Kiserikali inayosimamia Usalama wa Wafanyakazi Mahala pa kazi wameendelea kutambua ubora wetu katika utendaji" amesema Rwehumbiza.

Kwa upande wake Mfanyakazi wa kiwanda cha AtoZ Bakari Hashim ameushukuru uongozi wa kiwanda hicho kuweka mazingira ya kazi salama.

"Kitu ningependa kuomba kiwanda kiangalie ni namna ya kutuongezea mshahara walau upande kidogo, kwa sababu maisha yanapanda kila siku kwa hiyo unajikuta unachokipata hakilingani na matumizi" ameomba Hashim.

Wafanyakazi wa AtoZ wakiingia kwa maandamano katika uwanja wa kumbukumbu ya Shekh Amri Abeid Jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango akimwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Mhandisi Rwehumbiza kiwanda cha AtoZ kimeajiri wafanyakazi wengi kutoka Kanda ya Kaskazini na hata nje ya Kanda hiyo hatua inayosaidia kuinua uchumi wa watanzania wengi.

Amesema pia kiwanda kina maundombinu ya kisasa ya kusafishia majitaka yanayozalishwa kiwandani hapo na kimekuwa kikipata cheti cha ubora kutoka Baraza la udhibiti wa Mazingira NEMC.

Mhandisi Rwehumbiza amesema AtoZ imekuwa ikijali Afya za Wafanyakazi na wananchi wanaozunguka kiwanda hicho, hivyo wamekuwa wakihakikisha wanatii Sheria za nchi kwa kutunza mazingira.



This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post