Daladala walalamika kushuka biashara baada ya CORONA

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Madereva wa mabasi madogo ya abiria maarufu kama daladala wamelalamikia kushuka kwa biashara hiyo mara baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa mlipuko wa homa kali ya mapafu COVID-19.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti madereva hao wamesema kutokana na agizo la kuepuka msongamano ili kuthibiti kuenea kwa ugonjwa huo, wamelezimika kubeba abiria wachache tofauti na kipindi cha nyuma.

“Sasa hivi ni mwendo wa level seat (akimaanisha hakuna kusimamisha abiria ndani ya gari), hatua hii imeshusha makusanyo yetu ya kila siku kwa sababu abiria waliokuwa wakisimama walikuwa wanaongeza hesabu” Alisema Babuu Msemo dereva wa daladala kituo cha Kilombero.

Kauli hiyo iliungwa mkono na dereva mwenzake anayefanya safari za mjini-Njiro Salim Njoya ambaye alisema licha ya kubeba abiria kwa idadi ya viti vya gari lakini pia hawaruhusiwi kubeba abiria wa njiani kwani kila anayepanda anapaswa kunawa mikono.

“Unajua hili la kunawa mikono nalo limeleta shida, kwa sababu hata ukitaka kupakiza abiria wa njiani, wale waliopo ndani ya gari wanaanza kupiga kelele wakisema hajanawa mikono, na sisi hatutembei na maji kwenye gari, na hata ukiwa nayo ni kupoteza tu muda kuanza kuwanawisha njiani” Alisema Njoya

Walisema licha ya kuwa serikali ina nia njema ya kutaka kukabiliana na janga hilo lakini isingepiga marufuku kusimamisha abiria badala yake wangeweka utaratibu wa kila abiria kuvaa barakoa, na kunawa kabla ya kupanda ili kuinusuru biashara yao.

Kwa upande wa abiria wamefurahishwa na kitendo hicho kwani wamesema kwa sasa wanasafiri kwa uhuru na amani zaidi tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanajazwa kupita kiasi hali inayopelekea hewa kuwa nzito ndani ya gari.

“Wakati mwingine tunasafiri na wagonjwa au watoto wadogo, sasa ukikutana na daladala uliyojaza kupita kiasi ni changamoto, kama ni mtoto utashangaa anaanza kulia, na kama ni mgonjwa anazidishiwa tatizo’ Alisema Mama Aron.

Msimamizi wa kituo hicho cha daladala Joshua Lemomo amesema wamepokea maelekezo kutoka kwa wataalamu afya kuhakiklisha hakuna daladala itakayotoka standi ikiwa imebeba abiria zaidi ya idadi ya viti vilivyopo na kwamba wataendelea kusimamia agizo hilo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post