Dalili ya ugonjwa huu ni mbuzi na Kondoo kupanda joto,kuharisha,kutupa mimba na kufa.
Na mwandishi Wetu, Monduli
Mfuko wa uhifadhi wanyamapori (AWF) Jana limekabidhiwa dozi 30,000 za chanjo ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na Kondoo
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Shamba la mifugo la Manyara Ranchi wilayani Monduli ambapo zoezi la chanjo limezinduliwa.
Kaimu Afisa Mfawidhi wa kituo Cha magonjwa ya mifugo Kanda ya Kaskazini,Dk Raphael Mwampashi akizungumza katika hafla hiyo alisema shirika la chakula na dawa la umoja wa Mataifa (FAO ) limetoa dozi milioni 4 kwa lengo la kushirikiana na serikali kudhibiti ugonjwa huo.
DK. Mwampashi alisema wilaya ambazo zitapewa dozi hizo ni Monduli, Longido,Kiteto, Simanjiro,Ngorongoro,Kongwa na Serengeti.
"Huu ugonjwa ni hatari kwa mifugo na tumeanza kutoa chanjo hizi hapa manyara Ranchi kutokana na mifugo kuishi pamoja na wanyamapori wanaozunguka hifadhi za Taifa za Manyara na Tarangire ambao baadhi wanaweza kuambukizana"amesema
Afisa programu wa AWF ambao ndio wanasimamia Manyara Ranchi,Pastor Magingi amesema msaada huo wa chanjo ya sotoka ni msaada mkubwa kwao na wafugaji vijiji vya Esilalei na Oltukai ambavyo vinapakana na Shamba hilo.
Alisema kaya 1000 zenye kondoo na mbuzi 25,000 zitanufaika na chanjo hiyo ambayo pia itatolewa kwa mifugo iliyopo ndani ya Shamba hilo na hivyo kuzuia kusambaa ugonjwa huo kwa wanyamapori na mifugo.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Monduli,Kaiza Victor amesema chanjo hiyo itatolewa kwa vijiji vingine vya wilaya hiyo na wanatarajia kuchanja mifugo 350,000 na kuomba wafugaji kujitokeza kuchanja mifugo yao.
Meneja wa mifugo wa Manyara Ranchi,Lemaly ole Kibiriti alisema chanjo hiyo ya sotoka ya mbuzi na mifugo itazuia wanyamapori na mifugo kuambukizana.
Mwakilishi wananchi wa vijiji vinavyozunguka Shamba hilo,Lelia Medoti alisema msaada huo utawasadaia kudhibiti ugonjwa na akatoa wito wananchi kuchanja mifugo yao.