*Rekodi mpya yawekwa Mlima Kilimanjaro* *#Watalii wacheza Mchezo wa Vikwazo Kreta* *#Wateremka hadi chini kwa kukimbia

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro.

Kundi la watalii 45 kutoka mataifa 23 kote duniani limeweka rekodi mpya katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro kwa kufanya michezo ya kupita katika vikwazo kwenye eneo la kreta, pamoja na kushuka  kutoka katika kilele cha Uhuru kwa kukimbia.

Katika taarifa yake kwa umma, Kamishna mwandamizi wa uhifadhi,na mkuu wa Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete amesema watalii wanamichezo hao waliokuwa wakishiriki katika zoezi maalum la kuruka vikwazo kwenye maeneo yenye miinuko ya juu ambapo  waligawanyika katika makundi makuu mawili katika zoezi hilo lililochukua takribani siku tano.

"Kundi la kwanza lilipanda Mlima Kilimanjaro kwa utaratibu wa kawaida hadi kilele cha Uhuru na kushuka chini kwa kukimbia na kufika katika eneo la Kreta walilolitumia kucheza michezo mbalimbali ya kuruka vikwazo,"ilisema taarifa hiyo.

Na kuongeza,"Aidha, kundi la pili nalo lilipanda kwa utaratibu wa kawaida, na baada ya kufika kilele cha Uhuru walishuka chini hadi katika Lango la Mweka kwa kukimbia,".

Shelutete amesema "Michezo hii ambayo imefanyika kwa mara ya kwanza kwenye Mlima Kilimanjaro inafahamika duniani kama Altitude Obstacle Course Races  World Championships, ililenga  kuunganisha pamoja watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani kushiriki utalii wa michezo kwa pamoja ambayo pia ni mojawapo ya bidhaa za utalii zinazopatikana katika Hifadhi ya Kilimanjaro,".

 

Waanzilishi wa michezo hiyo David  Pickles na Rob Edmond wamesema michezo ya mwaka huu imefanikiwa sana kwa kuwa Mlima Kilimanjaro unazo sifa zote za kimsingi za kuwezesha kutimia kwa malengo ya  michezo hii. Wameamua kuwa litakuwa ni tukio la kila kwaka kwa Mlima Kilimanjaro ambapo watu kutoka mataifa yote duniani wataalikwa kushiriki.

 

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post