WANANCHI LOLIONDO WALALAMIKA ARDHI YAO KUVAMIWA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella akishiriki zoezi la kuchimba shimo kwaajili ya kuwekea alama (Beacoans) katika eneo la Kilometa za Mraba 1500 Loliondo

 

Na Mwandishi Wetu, Loliondo

Kufuatia zoezi linaloendelea la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la pori tengefu la Loliondo (Loliondo Game Controlled Area), Wananchi wanazounguka eneo hilo wameshangazwa na hatua hiyo ya Serikali na kudai kuwa zoezi hilo linafanywa bila ridhaa yao.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema eneo hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1500 limepunguzwa kutoka tarafa ya Loliondo na Sale lililokuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 4000 kabla ya kupunguzwa na serikali na kwamba kinachofanywa ni kuwapokonya wananchi ardhi yao.


Hata hivyo wamesema kwa kuwa wananchi wenyewe hawajakubaliana na zoezi hilo bado kuna meza ya majadiliano inaweza kufanyika kati ya wananchi wanaozunguka eneo hilo na Serikali ili kufikia muafaka.


“Sisi wananchi hatujakubaliana na hii hatua ya serikali ya kugawa eneo letu, wanasema wanapunguza eneo la kilometa za mraba 1500 na kutubakizia 2500, kwa makubaliano gani? kama wanataka eneo letu ni vyema wakaja tuzungumze,”anasema Melau ole Olobikoki.


Melau anasema eneo hilo wamekuwa wakilimiliki kihalali kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa ardhi ya mwaka 1923 na mabadiliko ya sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 ambayo ilitamka wazi kuwa vijiji vitapewa hatimiliki ya Ardhi na wao wanazo hati hizo.


“Kwa kweli tunashangazwa na hatua ya Serikali kulivamia na kuanza kulipunguza eneo letu  tunalomiliki kihalali bila ridhaa yetu na mbaya zaidi inafanya hivyo huku ikitambua inavunja sheria inayozisimamia yenyewe,”anasema.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella mpango wa Serikali ni kupunguza eneo la kilometa za mraba 1500 kulifanya kuwa hifadhi pekee na kwamba hakuna mwananchi hata mmoja ambaye ataondolewa katika maeneo hayo.


Mongella amesema eneo la Loliondo ni ekolojia muhimu ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti lakini pia ndio mazalia ya wanyamapori wengi hivyo Serikali inataka kulitunza eneo hilo kwaajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Aidha Mkuu huyo Mkoa amesema kuwa tafiti mbalimbali zinasema eneo hilo ndio chanzo cha maji yanayotumika na wakazi wa tarafa ya Loliondo lakini pia maji hayo hutiririka kuelekea mto Mara unaotumiwa na wanyama katika hifadhi ya Serengeti na Masai Mara nchini Kenya.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post