Mahakimu Wapya watakiwa kujiandaa kuendesha pikipiki


Dar es Salaam. 

Mahakimu wakazi wapya wanawake wametakiwa kujiandaa kuvaa jinsi ili kukabiliana na hali ya miundombinu ya maeneo ambayo watapangiwa hususani ya vijijini.

Sambamba na hilo, pia wametakiwa kuanza mazoezi ya kujifunza kuendesha pikipiki kwa kuwa kuna maeneo ambayo watalazimika kutumia usafiri huo.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi Julai 16, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alipowaapisha mahakimu wakazi wapya 20.

Amesema kuna maeneo ambayo mahakimu hao watapaswa kutumia pikipiki na kwa sababu wanawake ndio wengi siku hizi, waanze kutafuta majinsi ya kuvaa, kwa sababu pikipiki zipo na wananchi wanataka huduma za mahakimu.

Katika kulisisitiza hilo, ametolea mfano wa kijiji cha Nanjilinji, kilichopo Kijiji cha Nanjilinji, Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi, amesema wanakijiji husafiri zaidi ya kilimometa 100 kwenda mahakama ya mwanzo.

“Hivyo itabidi tuanze mazoezi ya pikipiki, tutavaa jinsi na tutapeleka haki kule. Wanawake si mpo, mpo tayari, eeeh!!

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vilevile ipo tayari kuwapokea na kupokea huduma za utoaji wa haki ambazo mtazitoa, kwa hiyo tujitayarishe kufanya kazi katika sehemu yoyote ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Juma.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani, kulikuwa na jumla ya mahakimu wakazi 1,115 lakini kwa uapisho wa mahakimu wakazi hao leo, sasa kutakuwa na mahakimu 1,135, wanaume wakiwa 540 na wanawake 575.

Wakati hali ikiwa hivyo, Jaji Mkuu amefafanua kuwa katika kiapo cha mahakimu hao, walitaja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo watapewa nafasi ya kufanya kazi sehemu yoyote nchini yenye kilometa za mraba zaidi 945,000.

“Kuna maeneo ambayo ni magumu, lakini kwa sababu mliapa kwamba mtalinda na kutetea katiba ya wale waliowatuma basi mtakwenda kule kwa sababu sehemu yoyote ambayo kuna watu wanastahili kupata huduma,” amesema Jaji Juma.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post