Aljazeera Yaisifu Tanzania kuboresha Mazingira ya Kazi kwa Wanahabari

Na Seif Mangwangi 


Shirika la Utangazaji la kimataifa la Aljazeera limepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita kuboresha mazingira ya uandishi wa habari nchini ikiwemo sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kuminya uhuru wa habari.

Pia shirika hilo limekubali , kushirikiana na Taasisi za Kihabari nchini ikiwemo Chama Cha wafanyakazi katika wa Vyombo vya habari Tanzania(JOWUTA) kutoa mafunzo kwa wanahabari ya usalama kazini na uandishi wa habari za uchunguzi.


Akizungumza katika Mkutano ulioandaliwa na shirikisho la kimataifa la waandishi wa habari Afrika (IFJ) ikiwa ni mfululizo wa vikao vya pembeni vinavyoendana na Kikao cha 77 Cha Tume ya Afrika ya  Haki za Binaadamu na Watu(ACHPR) ambavyo vinaendelea jijini Arusha, Mkurugenzi wa Aljazeera wa masuala ya jamii na Haki za Binaadamu,Sami Elhag amesema Tanzania ni nchi ya kuigwa.

Pia amesema aljazeera ipo tayari kusaidia wanahabari Tanzania ili kufanya kazi kwa ufanisi na miongoni mwa maeneo ambayo wataweza kusaidia ni mafunzo kwa wanahabari katika masuala ya usalama, jinsi ya kuandika habari za uchunguzi lakini pia ya kuboresha Utendaji wa kazi na kubadilishana uzoefu.


Alisema wanahabari Duniani wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama na tayari kituo cha aljazeera wanahabari wake wamepatwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kufungwa.


Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma alisema, wanahabari wanakabiliwa na changamoto za kiusalama wakiwa kazini hasa wanapokwenda kuandika habari sehemu zenye migogoro,maslahi duni na wengi hawana ujuzi wa kutosha  wa uandishi wa habari za uchunguzi na Vita na kukabiliana na majanga.


Awali Katibu wa IFJ Louis Thomasi alisema wanahabari maeneo mengi Duniani wanakabiliwa na changamoto za kiusalama kazini lakini pia na uwepo wa sheria ambazo ni kandamizi.


Amesema kuna haja ya wanahabari kupatiwa mafunzo ya kiusalama lakini kupatiwa huduma muhimu ikiwepo maslahi na kuwepo sheria ambazo zitakuza Uhuru wa Vyombo vya habari na Uhuru wa kujieleza.


Thomasi alitaka Serikali barani Afrika kuwa na sheria rafiki ambazo zinasaidia wanahabari kufanya kazi vizuri na hivyo kuchangia ukuaji wa demokrasia na Maendeleo.


Awali Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la A19, Alfred Bulakali alisema hakuna Demokrasia  kwenye taifa lolote bila kuwepo Uhuru wa Vyombo vya habari na Uhuru wa kujieleza.


Bulakali alisema Uhuru wa Vyombo vya habari ni oxygen ya demokrasia hivyo ni muhimu serikali barani Afrika kutoa Uhuru kwa vyombo vya habari.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo , Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Rodney Thadeus alisema serikali ya Tanzania imeboresha mazingira ya wanahabari kufanyakazi na Uhuru wa kujieleza.


Thadeus alisema Rais wa Tanzania,Dk Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuingia madarakani alitaka kupitiwa sheria za habari na kuboresha zoezi ambalo linaendelea vizuri.


Alisema kwa wanahabari Tanzania wamehakikishiwa Uhuru wa kufanyakazi lakini pia kwa kutokana na maboresho ya sheria makosa ya kitaaluma.yameondolewa kuwa ya kijinai,kutakuwa na baraza huru la habari na kuanzishwa Mfuko wa kusaidia wanahabari kielimu .


"Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa habari katika maboresho ya sheria na serikali inawahakikishia mazingira mazuri wanahabari"alisema


Akizungumza maombi ya mafunzo kwa wanahabari yaliyotolewa na JOWUTA , Thadeus alitaka mafunzo hayo kuhusisha pia maafisa habari wa Serikali.


"Suala la mafunzo na kubadilishana uzoefu linapaswa pia kuwafikia maafisa habari ambao ndio wanafanya kazi na waandishi lakini pia wengi wao ni waandishi na watangazaji ambao wanahitaji pia mafunzo"amesema.


Wakili Mary Mwita  na Wakili Mgusuhi Maswi kutoka Chama Cha Mawakili wa Umoja wa Afrika( PALU ) wakitoa mada zao walisema ni muhimu wanahabari kufanyakazi katika mazingira Salama wakiwepo Wanahabari wanawake ambao wamekuwa waathirika wa ukatili katika vyombo vya habari.


Wakili Mwita alisema, waandishi wanahabari wamekuwa wahanga wa ukatili hivyo ni muhimu kuendelea kujengewa uwezo lakini pia kuwepo na sheria ambazo zinawalinda.


Katibu wa Umoja wa waandishi wa habari nchini Kenya,(KUJ)  Erick Oduor alisema ni muhimu kuwepo na muongozo katika kusimamia masuala ya Ulinzi na Usalama kwa wanahabari.


"Kenya tayari tunamuongozo na tupo tayari kushirikiana na JOWUTA na wadau wengine kuwepo na muongozo kama huo katika nchi zao ili kuboresha Utendaji kazi kwa wanahabari"alisema.


Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa ,Mussa Juma aliwapongeza wanahabari kutoka nchi mbalimbali kushiriki mkutano huo na kuwahakikishia  watafurahi amani na Utulivu wa Tanzania.


"Mkutano wetu umekuwa mzuri sana tumejadiliana mambo muhimu kuboresha sekta ya habari Afrika lakini kubwa zaidi nashukuru Aljazeera kukubali kuja kusaidia wanahabari wa Tanzania"alisema.


Juma alipongeza serikali ya Tanzania kwa kuboresha Mazingira ya wanahabari kufanyakazi tofauti na nchi nyingine na kuahidi JOWUTA itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa habari kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi katika mazingira Salama.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post