Na Egdia Vedasto
Arusha
SERIKALI imekemea taasisi zilizozoko chini yake ambazo bado hazijajiunga na mfumo wa Serikali Mtandao (eGA) na kuagiza taasisi zote ambazo bado hazijajiunga zianze mara moja kwa kuwa zinakwamisha jitihada za Serikali za kuunganisha taasisi hizo katika mfumo mmoja.
Agizo hilo limetolewa leo Februari 6, 2024 na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene wakati akifungua Mkutano wa nne wa kikao kazi cha Mamlaka ya Serikali Mtandao.
Simbachawene amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya serikali kujiendesha kidijitali ili kurahisisha huduma muhimu kwa jamii hivyo taasisi ambazo zinasita kujiunga zinakwamisha malengo ya Rais na kufanya hivyo ni kosa.
"Taasisi zote za serikali zinatakiwa kuzingatia Sheria, viwango na miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kujiunga na serikali mtandao ili kuendana na mabadiliko ya kidigitali na nafikiri katika kikao kingine kuwe na ushindani ili kujua ni taasisi gani inafanya vizuri zaidi ya nyingine kidigitali na kutoa zawadi,"amesema.
Simbachawene amesema mfumo huo utasaidia kuzuia upotevu wa mapato ya serikali sanjari na kusaidia wananchi kupata huduma sahihi na kwa wakati katika taasisi mbalimbli nchini na kuepusha changamoto za foleni na kuzorota kwa huduma.
"Mfumo huu uliopo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari utazuia udurufu, utapunguza rushwa na kuzuia upotevu wa pesa za Umma, ndio sababu tunashangaa kuona kuna watendaji wa taasisi za Serikali bado hawajajiunga na mfumo huu, hatujui wana malengo gani"amesema Simbachawene.
Aidha Waziri Simbachawene ameziagiza taasisi zote nchini kufanya manunuzi na malipo yote kwa njia ya Serikali mtandao ili kuepuka ubadhilifu na upotevu wa pesa za Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba, amesema mfumo wa Serikali mtandaoni utarahisisha kubadilishana taarifa serikalini na kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi.
Amesema Idara ya mahakama imejitahidi kufanya vizuri katika matumizi ya Serikali mtandao na utaratibu huo umesaidia kupunguza foleni ya wateja wanaosubiri kusikilizwa kesi zao tofauti na hapo awali ambapo mfumo huo haukuwepo.
"Taasisi zote zitatakiwa kusomana ili kurahisisha utendaji kazi serikalini lakini pia kuokoa muda....hii itasaidia pia kuondoa ukiritimba wa mtu mmoja kusubiriwa kuweka saini kwenye nyaraka nyingi kwa kuwa ataweza kuifanya hiyo kazi hata akiwa mbali" Amesema Ndomba.
Pia amesema mamlaka
ya Serikali Mtandao imefanikiwa kujenga mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA ya
Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa, ujulikanao kama Government
Enterprises Service Bus (GoVESB), ambapo tayari taasisi za umma 109 zimeunganishwa na mifumo
117 imesajiliwa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Dkt Jasmine Tiisekwa amesema bodi yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mfumo huo na kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali yanafikiwa.
Zaidi ya wadau 1,000 wa Serikali Mtandao, kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma wakiwemo, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA, Maafisa TEHAMA pamoja na watumiaji wengine wa TEHAMA katika taasisi hizo wanashiriki mkutano huo.
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao katika taasisi za umma, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma.